Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Julai, 2020 amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Mhandisi Marwa Mwita Rubirya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Anthony Damian Sanga kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Dkt. Sief Abdallah Shekalaghe kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Allan Herbert Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Nadhifa Sadiki Kemikimba kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Dkt. Mwinyi Talib Haji kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia Wakuu wa Mikoa wakiwaapisha Wakuu wa Wilaya aliowateua katika Mikoa yao ambapo Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Robert Gabriel Luhumbi amemuapisha Bw. Fadhili Mohamed Juma kuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Aboubakar Kunenge amemuapisha Bw. Mussa Ramadhan Chogero kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka amemuapisha Bw. Aswege Enock Kaminyoge kuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Joachim Wangabo amemuapisha Bw. Calorius Constantine Misungwi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghwira amemuapisha Dkt. Athumani Juma Kihamia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rombo.
Wateule wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya ambao ni Bw. Bashir Paul Mhoja (Iringa), Bw. Ramadhan Salmin Possi (Chalinze), Bw. Baraka Michael Zikatimu (Urambo), Bw. John John Nchimbi (Babati), Bw. Emmanuel Matinyi Johnson (Kishapu) na Bw. Solomon Isack Shati (Hanang).
Pia, Makatibu Tawala wa Wilaya ambao ni Bi. Hanan Muhamed Bafagil (Arusha), Bw. Omary Mwanga (Nachingwea) na Bw. Saitoti Zelothe Stephen (Mbeya).
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi hao kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa kuzingatia viapo vyao na kwamba Watanzania wana matarajio makubwa nao.
Mhe. Rais Magufuli amemuelezea kila kiongozi aliyeteuliwa na ametaka waende wakashirikiane na viongozi wengine katika maeneo waliyopangiwa ili kuwatumikia vizuri wananchi hasa kutatua kero zinazowakabili na kuimarisha upatikanaji wa huduma.
Ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa juhudi kubwa za kuimarisha mazingira ya utalii hapa nchini hali inayowavutia watalii wengi kuja kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo licha ya kuwepo ugonjwa wa Corona (Covid-19).
Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania ni salama na wanaotembelea Tanzania wanakuwa salama. Amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa jitihada mbalimbali za kuimarisha usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Chamwino
20 Julai, 2020