Na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa shilingi bilioni 10 ili ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinziwa Taifa uanze eneo la Kikombo, Wilaya ya Chamwino, Dodoma. Rais Magufuli amesema kuwa uamuzi wa kujenga Makao Makuu hayo Jijini Dodoma ni jambo la kizalendo ambalo linatimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu Dodoma.
“Mwaka 2015 wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 nilitoa ahadi ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi Dodoma ili kutimiza ndoto ya miaka zaidi 40 ya Baba wa Taifa, sasa imetimia na jeshi limehamia Dodoma,”alisema Rais Magufuli.
Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa Jeshi la Wananchi limesaidia sana kuleta amani na si kwa Tanzania tu bali Lebanon, Uganda, Jumhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchini nyingine nyingi Duniani.
Akiweka jiwe na msingi la ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Rais aliamuru maandalizi ya ujenzi ya barabara ya kuelekea eneo hilo yaanze wiki ijayo ili barabara ijengwe kwa kiwango cha lami.
Kuhusu fidia ya waliokuwa wakazi wa eneo ambalo limetwaliwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi huo, Rais Magufuli amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kuanza kuwalipa fidia kuanzia tarehe 1, Desemba, 2019.
Mkazi wa Kijiji cha Kikombo, Paul Andrew amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuagiza walipwe fidia na kuwajengea barabara kwa kiwango cha lami.
“Kwa kweli tunamshukuru Mhe. Rais kwa uamzi wake wa kutufidia kwani tumekaa miaka miwili bila kulima kwenye maeneo yetu na bila kulipwa chochote,” alisema Andrew.
Ujenzi huu ni wa kihistoria kwani tangu Uhuru wa Tanganyika, Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa unajengwa na Serikali ya Tanzania.