Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Apongeza Maamuzi ya Maalim Seif
Jan 15, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Maalum – CHATO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Shariff Hamad kwa uamuzi wake wa kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, jambo lililochangia kudumisha amani, umoja na mshikamano visiwani Zanzibar.

Mheshimiwa Rais ametoa pongezi hizo jana wilayani Chato alipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad.

“Ni maamuzi ya kishujaa, ni maamuzi yenye muelekeo na muongozo wa Mwenyezi Mungu, tumeona nchi nyingi zikishindwa kuendelea kwasababu ya ugomvi, na wakati mwingine ugomvi unachochewa na watu wa nje” amesema Rais Magufuli

Aidha, Mheshimiwa Rais amesema uamuzi uliofanywa na viongozi hao wa ngazi za juu visiwani Zanzibar umesababisha kumalizika kwa ubaguzi baina ya Wapemba na Waunguja.

“Nimeanza kuuona mwanga wa maendeleo ya Zanzibar, na nimeanza kuyaona maendeleo ya Tanzania, kwasababu hakuna Zanzibar bila Tanzania na hakuna Tanzania bila Zanzibar” amesema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, Mheshimiwa Rais amewataka Wazanzibari na Watanzania wote kutoyumbishwa na tofauti za kisiasa na badala yake watangulize maslahi ya Taifa mbele.

 “Mambo ya vyama yasitusumbue, tunatakiwa sisi watanzania tutangulize maslahi ya Taifa letu kwanza, maadui zetu wangefurahi sana kuona tunagombana lakini wameshindwa kwasababu nyinyi kina maalim seif hamutaki hivyo” amesema Rais Magufuli.

Sambamba na hayo, Mheshimiwa Rais amempongeza Dkt. Mwinyi kwa utumishi uliotukuka aliouonesha mwanzoni mwa uongozi wake na kumtaka Maalim Seif kutumia uzoefu wake kumshauri Rais wa Zanzibar.

“Nimewahakikishia ushirikiano wa Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa maendeleo ya Wazanzibari, sitawaacha kamwe, kwasababu nyote mnahubiri amani, Rais Mwinyi anahubiri amani, Maalim Seif anahubiri amani, wazanzibari wote wanahubiri amani” amesema Mheshimiwa Rais.

Hii ni ziara ya kwanza ya viongozi wa juu visiwani Zanzibar tangu walipoingia madarakani Novemba 2020.  

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi