Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli ampongeza Rais Mnangagwa, Atoa Wito kwa Jumuiya ya Kimataifa Kuondoa Vikwazo Dhidi ya Zimbabwe
May 29, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_43624" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati wa Dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Mwenyeji wake Rais wa Zimbabwe Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa Ikulu ya Harare nchini Zimbabwe. Mei 28, 2019.[/caption] [caption id="attachment_43623" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Mwenyeji wake Rais wa Zimbabwe Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa kwa Dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa Ikulu ya Harare nchini Zimbabwe. Mei 28, 2019.[/caption]

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa kwa hatua madhubuti za kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi hiyo na ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 28 Mei, 2019 wakati akitoa hotuba katika Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Rais Mnangagwa kwa heshima yake na kufanyika Ikulu Jijini Harare.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi kifupi cha tangu Mhe. Rais Mnangagwa aingie madarakani hali ya uchumi imeanza kuimarika ambapo kwa sasa uchumi wa Zimbabwe unakua kwa wastani wa asilimia 3.5, mwaka ujao unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 na mwaka unaofuata kuongeza hadi wastani wa asilimi 4.4.

Kufuatia hali hiyo ameisihi Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe kwa kuwa vikwazo hivyo vinawaumiza wananchi wa Zimbabwe wakiwemo watoto na wanawake.

[caption id="attachment_43620" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi zawadi ya picha Mwenyeji wake Rais wa Zimbabwe Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa inayoonyesha baadhi ya Wanyama waliopo katika Hifadhi mbalimbali za Wanyama Tanzania pamoja kabla ya kuanza mazungumzo katika Ikulu ya Harare Zimbabwe. Mei 28, 2019.[/caption]

Katika hotuba hiyo, Mhe. Rais Magufuli kwa mara nyingine amewapa pole Rais na wananchi wote wa Zimbabwe kwa kupoteza watu takribani 400 waliofariki dunia katika mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai kilichoikumba Zimbabwe Machi 2019. Amesema Watanzania wanaungana na ndugu zao Wazimbabwe katika majonzi ya kuondokewa na jamaa zao na wanawaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amina.

Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Zimbabwe ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mzee Robert Mugabe, Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania inatambua na inathamini uhusiano huu wa kihistoria na kidugu na amebainisha kuwa jukumu lililopo sasa ni kuelekeza nguvu nyingi zaidi katika uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi utakaoziwezesha Tanzania na Zimbabwe kuongeza biashara na uwekezaji.

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa katika mazungumzo yake ya faragha na Mhe. Rais Mnangagwa leo mchana wamekubaliana kusimamia ipasavyo makubaliano yaliyopo katika Kamati ya Pamoja ya Kudumu (Joint Permanent Commission – JPC) kwa manufaa ya nchi zote mbili.

[caption id="attachment_43619" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyeji wake Rais wa Zimbabwe Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa, Mke wa Rais wa Zimbwabwe Mhe. Amai Mnangagwa(Wapili kutoka kulia),Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi (Wapili kutoka kushoto),Waziri wa Mambo ya nje wa Zimbabwe Mhe.Sibusiso Moyo(Wakwanza kulia) pamoja na Mkuu wa Itifaki wa Tanzania Balozi Grace Martin kabla ya kuanza mazungumzo katika Ikulu ya Harare Zimbabwe. Mei 28, 2019.[/caption]

“Mhe. Rais Mnangagwa ujio wangu hapa Zimbabwe ni kuthibitisha kuwa urafiki wetu bado upo imara na sisi Tanzania tumejipanga kuuimarisha zaidi, tunataka tufanye biashara zaidi na nyinyi ndugu zetu wa Zimbabwe ili tukuze uchumi wa nchi zetu na kuongeza kipato cha wananchi wetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Mnangagwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake, na amemthibitishia kuwa yeye na wananchi wa Zimbabwe wanatambua kuwa Watanzania ni ndugu zao waliojitolea kwa dhati katika ukombozi wao wakiongozwa na dhamira ya dhati ya Hayati Mwl. Nyerere.

Amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi wa kwanza katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi wakati Zimbabwe alipokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai mwezi Machi 2019.

Mhe. Rais Mnangagwa amesema msaada huo uliwagusa Wazimbabwe wengi na kuwakumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na mabadiliko ya tabia nchi.

[caption id="attachment_43616" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Zimbabwe Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa pamoja Mke wa Rais wa Zimbwabwe Amai Mnangagwa kabla ya kuanza mazungumzo katika Ikulu ya Harare Zimbabwe. Mei 28, 2019.[/caption]

Amesisitiza kuwa daima Zimbabwe itabaki kuwa rafiki na ndugu wa kweli wa Tanzania na hivyo amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa kuongeza biashara na uwekezaji pamoja na kushirikiana katika usafiri wa anga.

Amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumpa mbinu mbalimbali za kiuongozi ikiwemo kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali na ameahidi kudumisha ushirikiano kati ya chama chake ZANU-PF na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dhifa hiyo ya Kitaifa imehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Zimbabwe Mhe. Constantino Chiwenga, Mke wa Rais wa Zimbabwe Mhe. Amai Auxillia Mnangagwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndg. Philip Mangula, viongozi wa ZANU-PF, Mawaziri wa Tanzania na Zimbabwe na Mtoto wa Baba wa Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Ndg. Makongoro Nyerere.

Kesho (29 Mei, 2019), Mhe. Rais Magufuli atamaliza ziara yake hapa nchini Zimbabwe kwa kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Mnangagwa na kutembelea na kuweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu ya mashujaa wa ukombozi wa Zimbabwe.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Harare

28 Mei, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi