[caption id="attachment_36121" align="aligncenter" width="560"] Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wajasiriamali wa feri (hawapo pichani) jana jijini Dar es Salaam [/caption]
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Oktoba, 2018 ameahidi kutoa shilingi Milioni 20 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ofisi ya wajasiriamali wa eneo la Feri katika Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam na ameahidi kufanyia kazi changamoto mbalimbalizinazowakabili katika shughuli zao.
Mhe. Rais Magufuli amekutana na Wajasiriamali hao ambao wanajumuisha Wavuvi Wadogo na Mamalishe wakati akiwa katika mazoezi ya jioni pamoja na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ambaye pia amewachangia wajasiriamali wanawake shilingi Milioni 5.
Pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli, wajasiriamali hao wameomba awasaidie wasifukuzwe na Manispaa ya Ilala katika eneo hilo, na badala yake wawekewe utaratibu mzuri wa kufanya biashara zao.
Pia wameomba waondolewe ushuru unaotozwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kwa mitumbwi ya wavuvi wadogo wa samaki, kama ambavyo Serikali imewaondolea ushuru wakulima wanaopeleka sokoni mazao yasiyozidi tani moja.
Aidha, Wajasiriamali hao wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri ya kuiongoza nchi na kushughulikia kero za Watanzania ikiwa ni pamoja na kuwatembelea na kuwasikiliza kwa mara ya pili.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi maombi ya Wajasiriamali hao na amewapongeza kwa juhudi zao za kujitafutia kipato.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Oktoba, 2018