Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Akagua Maendeleo ya Ujenzi wa Msikiti BAKWATA
Feb 28, 2020
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Februari, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti mkubwa wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa Kinondoni Jijini Dar es Salaam.

Msikiti huo unajengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco baada ya kuombwa na Mhe. Rais Magufuli alipofanya ziara rasmi hapa nchini Oktoba 2016.

Akiongozwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally, Mhe. Rais Magufuli amejionea kazi za ukamilishaji wa jengo jipya la Msikiti na jengo la ofisi ya Taasisi ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco zikiendelea kukamilishwa, na ameelezea kufurahishwa kwake na ubora na uzuri wa Msikiti huo.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mfalme Mohammed VI wa Morocco kwa kutekeleza ombi alilomuomba la kuwajengea Waislamu Msikiti mkubwa kuliko yote hapa nchini, na amempongeza Mufti wa Tanzania na Waislamu wote kwa kujengewa nyumba nzuri ya Ibada.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwajali Waislamu na kuwaombea msaada wa kujengewa Msikiti huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 97.

Akiwa na viongozi wenzake wa BAKWATA, Sheikh Mkuu Aboubakar Zubeir bin Ally ameongoza Dua ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli na kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aiepushe Tanzania dhidi ya maradhi ya homa ya virusi vya corona, kudumisha amani na utulivu na kuombea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu ufanyike vizuri na kwa amani.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

28 Februari, 2020

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi