Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Akabidhi Uenyekiti wa SADC
Aug 17, 2020
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Agosti, 2020 amekabidhi uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi baada ya kuongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.


Makabidhiano hayo yamefanyika katika mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao kwa kuwaunganisha viongozi wakuu 16 kutoka nchi wanachama ambapo Mhe. Rais Magufuli amekabidhi uenyekiti akiwa Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.


Katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Jamhuri ya Botswana Mhe. Mokgweetsi Masisi amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ) na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Matemela Cyril Ramaphosa amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC Organ.


Akizungumza kabla ya kukabidhi uenyekiti wa SADC, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi zote wanachama wa SADC kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake ambapo SADC imepiga hatua kubwa katika kutimiza malengo yake makuu.


Mhe. Rais Magufuli ameyataja baadhi ya maeneo ambayo yamepata mafanikio makubwa wakati wa uongozi wake kuwa ni kuendelea kusimamia amani, ulinzi, utawala bora na demokrasia ambapo licha ya kuwa Jumuiya iliyokuwa na amani zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine, nchi 5 za Botswana, Msumbiji, Namibia, Mauritius na Malawi zimefanya uchaguzi kwa amani.


Eneo jingine ni kuimarisha utengamano wa kiuchumi ambapo mfumo wa kutambua asili ya bidhaa (e-certificate on rules of origin) umeanzishwa, Baraza la Biashara la SADC limeanzishwa, megawati 3,595 za umeme zimeongezwa na kuingizwa katika gridi za nchi wanachama, na pia Tanzania/Zambia na Malawi/Msumbiji zimeingia katika makubaliano ya kusafirisha umeme.


Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita SADC imeweza kutengeneza ajenda mpya za ndani ya Jumuiya ambapo Dira ya SADC ya mwaka 2050 imeandaliwa na pia mpango elekezi wa maendeleo ya kikanda wa 2020 – 2030 umekamilika.


Mafanikio mengine ni kusimamia kwa ukaribu uondoaji wa vikwazo dhidi ya Zimbabwe, kuingiza lugha ya Kiswahili kuwa miongozi mwa lugha 4 rasmi za SADC na kuiongoza Jumuiya bila kutetereka katika kipindi kigumu cha janga la virusi vya Corona (Covid-19) ambapo Tanzania iliendelea kuzihudumia nchi wanachama likiwemo jukumu muhimu la kusambaza dawa za binadamu.


Wakuu wa Nchi na Serikali wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake wa mwaka mmoja ambapo SADC imepiga hatua kubwa na wameahidi kuendeleza juhudi kubwa alizozianzisha katika kusimamia ajenda za Jumuiya kwa ustawi wa uchumi, ulinzi, usalama, amani, ustawi na ustawi wa wananchi.


Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki mkutano huo pia wametoa salamu za pole kwa Mhe. Rais Magufuli na Watanzania wote kwa kuondokewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa ambaye wamemuelezea kuwa alikuwa kiongozi hodari aliyeipenda SADC na kuzisimamia vizuri ajenda za Jumuiya hiyo hata baada ya kustaafu uongozi wake.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
17 Agosti, 202

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi