Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Aitaka Bodi ya NMB kuangalia Upya Gawiwo Linalotolewa kwa Serikali
Apr 23, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_30800" align="aligncenter" width="811"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza kuhusu umuhimu wa uwekezaji uliofanywa na mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa kujenga jengo lenye gorofa 11 mjini Dodoma wakati wa hafla ya kuzindua jengo hilo na Tawi jipya la Benki ya NMB lijulikanalo kwa jina la Kambarage.[/caption]

Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Bodi ya National Microfinance Bank (NMB) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo kuangali kiasi cha gawiwo kinachotolewa na benki hiyo, kutokana na kiasi hicho kutoongeza ndani ya miaka mitatu mfululizo.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Mjini Dodoma wakati alipokuwa akifungua jengo jipya la Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF) pamoja na tawi jipya la NMB Kambarage lililoko katika jengo hilo.

"Kuna mambo mazuri mengi yaliyofanywa na NMB lakini tunahitaji uhakiki wa gawiwo linalotolewa kwa Serikali, kutokana na gawiwo hilo kutopanda kwa miaka mitatu mfululizo tangu mwaka 2014/2015 mpaka mwaka 2016/2017 ambapo benki hiyo imekuwa ikitoa shilingi Bilioni 16.525 kama gawiwo la hisa ya asilimia 32 iliyonayo katika Benki hiyo," alisema Rais Magufuli.

Ameendelea kwa kusema, ni matumaini yake kuwa kiasi hicho cha fedha kitapanda kwa mwaka 2017/2018 kutokana na benki hiyo kutengeneza faida kila mwaka.

[caption id="attachment_30802" align="aligncenter" width="811"] Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuzindua tawi jipya la Benki ya NMB la Kambarage mjini Dodoma mapema leo.
[/caption] [caption id="attachment_30801" align="aligncenter" width="900"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuzindua jengo la PSPF lenye gorofa 11 mjini Dodoma mapema leo na Tawi jipya la Benki ya NMB linalojukulikana kwa jina la Kambarage ikiwa ni sehemu ya Kutambua mchango wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika ustawi wa Benki hiyo.
[/caption] [caption id="attachment_30803" align="aligncenter" width="900"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere picha ya Baba wa Taifa iliyotolewa na Benki ya NMB kwa familia hiyo ikiwa ni zawadi kwa kuenzi mchango wake katika kuendeleza Benki ya NMB.[/caption]

Aidha, Rais Magufuli ameipongeza benki ya NMB kwa kuwa na matawi mpaka vijijini pamoja na kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 3000 na kutoa misaada ya kijamii ikiwemo madawati 600, kompyuta 300 kwa shule za Sekondari na vitanda vya wagonjwa.

Vilevile Rais Magufuli ameupongeza mfuko wa PSPF kwa kuona fursa ya Serikali kuhamia Dodoma na kujenga jengo ambalo limeboresha na kupendezesha mandhari ya Dodoma ambapo pia ujenzi huo umetoa ajira kwa Watanzania takribani 250.

Pia amesema, mfuko huo umekuwa ukitoa mikopo kwa wanachama wake pamoja na kuwekeza katika ujenzi wa viwanda mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiwanda cha cha Sukari Kagera, kiwanda cha nguo na turubai vilivyopo mkoani Morogoro.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amesema Rais Magufuli kupitia TAMISEMI ametoa shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi mbalimbali wa miundombinu mkoani Dodoma.

Dkt. Mahenge ametaja miundombinu hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa stendi mpya ya kisasa yenye uwezo wa kuingia mabasi makubwa 250, magari madogo 600 pamoja na bajaji na bodaboda 300 kwa wakati mmoja.

Aidha, Dkt Mahenge ameitaja miundombinu mingine ambayo ni ujenzi wa soko la kisasa, sehemu ya kupaki malori, miundombinu ya majitaka, maeneo ya kupumzikia pamoja na kuboresha miundombinu ili kuondoa msongamano wa magari.

kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji ameutaja mfuko wa PSPF kuwa ndio mfuko wa kwanza kuwekeza katika vitega uchumi Makao Makuu ya Nchi ukiondoa mfuko wa LAPF ambao Makao Makuu yake yapo Mkoani Dodoma.

Jengo la PSPF ni moja ya majengo marefu yaliyoko mkoani Dodoma ambapo ina jumla ya ghorofa 11 pamoja na eneo la maegesho ya magari 161 ambapo mpaka sasa jengo hilo limeshapata wapangaji kwa asilimia 100.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi