Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Afungua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi Mapinga-Bagamoyo
Feb 06, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_28616" align="aligncenter" width="750"] Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akivuta utepe kuashiria ufunguzi wa Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi kilichopo Mapinga, Bagamoyo Mkoani Pwani. Wa Pili kushoto anayevuta utepe ni Naibu Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Mafunzo kutoka tume Kuu ya Kijeshi ya China, Meja Jenerali Yang Jian na wa kwanza kushoto anayepiga makofi ni Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Wang Ke[/caption]

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Februari, 2018 amezindua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi (Comprehensive Training Center – CTC) kilichopo Mapinga katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.

Kituo hicho kimejengwa kwa msaada kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 67.87 na kitatumika kutoa mafunzo ya kijeshi ya kisasa yatakayowawezesha askari kukabiliana na vitisho vya kiusalama vya kisasa.

Kabla ya kuzindua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli na Balozi wa China hapa nchini Mhe.  Wang Ke wameshuhudia makabidhiano ya kituo hicho kutoka Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China lililowakilishwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Utawala wa Kamisheni Kuu ya Jeshi hilo Jenerali Yang Jian kwenda kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililowakilishwa na Meja Jenerali Yakub Hassan Mohamed.

[caption id="attachment_28617" align="aligncenter" width="750"] Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi mara baada ya kufungua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi kilichopo Mapinga, Bagamoyo Mkoani Pwani.[/caption]

Mhe. Rais Magufuli pia ameshuhudia mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa katika kituo hicho yakiwemo shambulizi la kutokea baharini (amphibian landing), makomandoo kukabiliana na magaidi na kupiga shabaha kwa kutumia miundombinu ya kisasa.

Akizungumza na Maafisa, Askari na Wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la makabidhiano ya kituo hicho Mhe. Rais Magufuli amelishukuru Jeshi la Ukombozi la Watu wa China na Serikali ya China kwa kutoa msaada wa kujengwa kwa kituo hicho na amesema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kutambua mchango wa China katika Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli amesema China imeendelea kudhihirisha urafiki na udugu wake na Tanzania kwani licha ya kujenga kituo hicho pia imetoa msaada wa kujenga kituo cha mafunzo ya kijeshi ya anga cha Ngerengere Mkoani Morogoro na miradi mingine ya maendeleo ya jamii, na hivyo amemuomba Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping.

Mhe. Wang Ke na Jen. Yang Jian wamesema China imejenga kituo hicho cha mafunzo maalum ya kijeshi ambacho ni alama nyingine ya uhusiano na ushirikiano wa kirafiki na kidugu kati yake na Tanzania na wameipongeza JWTZ kwa kupata kituo ambacho wanaamini kitatumika kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.

[caption id="attachment_28618" align="aligncenter" width="750"] Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke mara baada ya kukifungua kituo hicho cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi.[/caption]

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesema miundo ya kituo hicho inakifanya kuwa kituo cha kimataifa kilicho bora zaidi Afrika Mashariki na Kati kitakachoweza kutoa mafunzo ya kisasa kwa askari wengi na amemuomba Mhe. Rais Magufuli kusaidia ujenzi wa daraja la mto Mpigi litakalokiunganisha na barabara ya kwenda Dar es Salaam.

Pamoja na kukubali ombi hilo Mhe. Rais Magufuli pia amekubali maombi ya Jen. Mabeyo ya kupeleka maji, umeme na barabara katika eneo ambalo China imekubali kutoa msaada wa kujenga makao makuu ya JWTZ Mkoani Dodoma na ameahidi kuziagiza wizara husika kutekeleza maombi hayo haraka.

[caption id="attachment_28620" align="aligncenter" width="750"] Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Makomandoo wa JWTZ ambao walishiriki katika mazoezi ya Kijeshi kabla ya ufunguzi wa kituo hicho.[/caption]

Tukio la kukabidhiwa kwa kituo cha mafunzo maalum ya kijeshi limehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mapinga waliosimamisha msafara wake na kumuomba awasaidie kulipwa fidia kufuatia maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya miradi, ukiwemo mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha mafunzo cha jeshi na kuvunjiwa nyumba zao katika eneo la Makurunge.

[caption id="attachment_28619" align="aligncenter" width="750"] Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Mapinga (hawaonekani pichani) waliokuwa wakiwasilisha kero mbalimbali za ardhi wakati alipokuwa akirejea jijini jijini Dar es Salaam mara baada ya kufungua kituo hicho cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi kilichopo Mapinga mkoani Pwani.[/caption]

Katika majibu yake Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haiwezi kurudia kuwalipa watu ambao tayari walishalipwa fidia na hawezi kuwatetea watu ambao wamevunja sheria kwa kuvamia maeneo yasiyokuwa yao.

Mhe. Rais Magufuli pia amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kutekeleza  mradi wa bandari na eneo la uwekezaji la Bagamoyo na amewataka watu wote waliolipwa fidia wakati hawakuwa na maeneo warejeshe fedha za Serikali, waliolipwa fidia kuondoka katika maeneo yaliyolipiwa, na kwa wale ambao hawajalipwa fidia waendelee kutumia maeneo yao kwa shughuli zao mbalimbali.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

06 Februari, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi