Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Dkt. Samia Aelekeza Milioni 960 za Maadhimisho ya Uhuru Kujenga Mabweni ya Wenye Mahitaji Maalum
Dec 05, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza jumla ya Shilingi milioni 960 zilizotengwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru kwa mwaka 2022 ziwasilishwe Ofisi ya Rais - TAMISEMI na zitumike kwa ajili ya kujenga mabweni katika shule Nane za msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Hayo yamezungumzwa leo Desemba 5, 2022 jijini Dodoma wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akitoa taarifa kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Waziri Simbachawene amesema kuwa, Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka 2022 yataadhimishwa kwa kaulimbiu inayosema "Miaka 61 ya Uhuru, Amani na Umoja ni Nguzo ya Maendeleo Yetu, kaulimbiu yenye lengo la kuonesha nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha uchumi unaojikita katika maendeleo ya watu kwa kufanya mabadiliko katika sekta zote za kiuchumi na kijamii ili kufikisha neema na maendeleo kwa wananchi wote wa Tanzania.

“Natumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua fedha hizo zitumike kwa ajili ya kujenga mabweni katika shule Nane za msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum ambazo ni Buhangija - Shinyanga, Goheko - Tabora, Darajani - Singida, Mtanga - Lindi, Songambele - Manyara, Msanzi - Rukwa, Idofi - Njombe na Longido – Arusha, hii ni dhamira ya dhati ya Rais wetu ya kuwajali na kuwajengea mazingira rafiki watu wenye mahitaji maalum hapa nchini," alisema Waziri Simbachawene.

Amefafanua kuwa, sherehe za mwaka huu hazitokuwa na gwaride wala shughuli nyingine za kitaifa na badala yake midahalo na makongamano mbalimbali yatafanyika katika wilaya zetu zote nchini kwa kujadili na kutafakari kwa pamoja na kukumbuka tulipotoka, tulipo na tunapoelekea kuhusu maendeleo endelevu ambayo nchi yetu imeyapitia na kuyafikia.

Aidha, midahalo na makongamano hayo yatatanguliwa na ratiba mbalimbali kwa viongozi wa mikoa na wilaya kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika maeneo ya kutolea huduma za kijamii kama hospitali, shule, nyumba za wazee, makundi yenye mahitaji maalum na katika maeneo yetu ya kuishi.

Vile vile, Ofisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya TAMISEMI itafanya usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya midahalo na makongamano hayo ili kujiridhisha na matokeo yake ambapo tayari zimetoa maelekezo kuhusu ratiba kwa ajili ya kurahisisha uendeshaji wa shughuli za maadhimisho kwa mwaka huu kwenye mikoa na wilaya zote nchini, hivyo amehamasisha wananchi wote kushiriki ipasavyo midahalo na makongamano katika idara zote na kujadili kwa kina kuhusu maendeleo endelevu katika miaka 61 ya Uhuru wa nchi yetu hasa kwa Tanzania Bara.

Kwa niaba ya Serikali na Kamati ya Maandalizi Kitaifa, Mhe. Simbachawene amewashukuru wananchi wote kwa kuendelea kudumisha amani nchini na kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi wote na amesisitiza kuwa ofisi zote za Serikali nchini zipambwe kwa Bendera za rangi ya Taifa na picha ya Rais wetu mbele ya ofisi zote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi