Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Dkt. Magufuli Azindua Kitabu cha Dkt. Mengi
Jul 02, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Juni 2018, amezindua kitabu chenye historia ya maisha ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dkt. Reginald Abraham Mengi kinachoitwa I CAN, I MUST I WILL jijini Dar es salaam.

Mhe. Rais Dkt. Magufuli amewataka wafanyabiashara nchini kuiga mfano wa Dkt Mengi na kupuuza maneno ya baadhi ya watu wanaowakatisha tamaa kwani hakuna serikali yoyote duniani iliyopata maendeleo bila ya kushirikiana na sekta binafsi.

Amesema hata Serikali imekuwa ikikatishwa tamaa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa Reli ya Kisasa, Utoaji elimu bila malipo, Ununuzi wa ndege mpya saba na ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Stiglers Gorge na mingine mingi.

Pamoja na kukatishwa tamaa huko na baadhi ya watu wasioitakia nchi maendeleo Serikali haikukata tamaa na imekuwa ikiendelea na utekelezaji wa miradi yake kwa lengo la kuwaletea watanzania maendeleo.

 ‘’Ninachotaka kuwaambia Wafanyabiashara wa Tanzania na watanzania kwa ujumla ni kuwa kitabu cha Mzee Mengi kiwe fundisho kwetu sote tunaweza kwelikweli,na mimi napenda nitoe wito kwa wafanyabiashara wote nchini ninarudia wito wangu msisikilize maneno ya watu wanaowakatisha tamaa fanyeni biashara zenu kwelikweli, wekeni uwekezaji wenu wote hakuna serikali inayoweza kuendelea bila kutegemea sekta binafsi’’ amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amsema watanzania wakiamua wanaweza kwani Dkt. Mengi alizaliwa katika familia masikini lakini kwa kuwa aliukataa umasikini ameweza kufikia maendeleo aliyonayo hivi sasa na hivyo kuwataka watanzania wote kujiamini na kuukataa umasikini kwani tunaweza.

Aidha Rais Magufuli amewataka Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kuwahamasisha wafanyabiashara katika nchi zao kuja kuwekeza hapa nchini kwani Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji.

Amesema katika historia ya mzee Mengi yapo mengi amekutana nayo ya kumkatisha tamaa lakini yeye hakukata tamaa bali aliamini anaweza na akaamua kufanya  na akaweza hivyo watanzania tuache kukatishana tamaa ili tuweze kufikia mafanikio ya kweli.

Dkt. Magufuli amesema Dkt. Reginald Mengi ni mfanyabiashara wa kuigwa hapa nchini kutokana na jitihada zake mbalimbali katika mchango wa Taifa kwa kuwa chanzo cha ajira kwa watanzania na kulipa kodi kwa serikali inayokwenda kutoa huduma mbalimbali kwa watanzania wote.

Kwa upande wake Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi amempongeza Dkt. Mengi kwa uamuzi wa kuandika historia ya maisha yake na kuonyesha hatua mbalimbali alizopitia hadi kufikia mafanikio aliyonayo kwani ni watu wachache wanaoweza kufanya kitu kama hicho hasa kwa Afrika.

Amesema ipo fikra kwamba watu wenye uwezo wa uandishi ni wale wenye taaluma na wasomi katika vyuo mbalimbali lakini Dkt. Mengi amevunja dhana hiyo na kuweza kuandika kitabu hicho.

Nae Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Dkt. Reginald Mengi amemshukuru Rais Dkt. John Pombne Magufuli kwa kukubali kumzindulia kitabu hicho na kuwataka watanzania kutokata tamaa katika kufikia hatua ya maendeleo kwani alichoandika yeye ni uhalisia wa maisha yake tangu akiwa masikini hadi kufikia mafanikio aliyonayo.

Dkt. Mengi amepata msukumo wa kuandika kitabu hicho cha historia ya maisha yake ili kutimiza azma ya marehemu mtoto wake Rodney Mutie Mengi aliyemtaka kuandika kitabu hicho na mambo mengine ambayo atayatimiza kadri awezavyo.

Jaffar Haniu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

02 Julai, 2018

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi