Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Profesa Mbarawa Asaini Mkataba wa Ushirikiano wa Pamoja wa Usafirshaji
Jul 28, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_7756" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akipitia mkataba wa makubaliano katika mkutano wa kwanza wa Mawaziri wa usafirishaji na uchukuzi mkoani Kigoma,kuhusu kushirikiana katika miradi ya maendeleo ya pamoja kati ya nchi ya Tanzania, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).[/caption]

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesaini mkataba wa ushirikiano katika miradi ya pamoja inayohusu masuala ya usafirishaji na uchukuzi, lengo likiwa ni kuleta maendeleo na kukuza uchumi katika nchi wanachama.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo mkoani Kigoma, Waziri Mbarawa amesema kuwa mkataba huo ambao unahusisha nchi ya Tanzania, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), unalenga kuhuisha fursa za kiuchumi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Amesema pamoja na mambo mengine, Mawaziri wa Muungano wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Nchi za Ukanda wa Ziwa Tanganyika (LTITS), wamepokea ripoti ya wataalam inayooelekeza utekelezaji wa miradi kwa nchi wananchama ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

[caption id="attachment_7757" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisaini mkataba wa makubaliano mkoani Kigoma, kuhusu kushirikiana katika miradi ya maendeleo ya pamoja kati ya nchi ya Tanzania, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).[/caption]

“Tumeelekeza Sekretarieti ya ukanda huu kuunganisha pamoja rasilimali kutoka nchi wanachama, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili miradi inayotekelezwa kwa pamoja iweze kukabiliana na changamoto za usafirishaji zilizopo katika ukanda wa Ziwa Tanganyika”, amesema Profesa Mbarawa.

Mawaziri hao Bagiire Aggrey Henry kutoka Uganda, Eng. Jean Bosco Ntunzwenimana kutoka Burundi na Katibu wa Sekretarieti wa Ukanda huo Capt. Dieudonne Dukundane kwa pamoja  wamepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania hususan katika ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), na uboreshaji wa huduma katika Mamlaka ya Bandari Tanzania ambavyo kwa pamoja vitaunganisha Ukanda huo.

[caption id="attachment_7758" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma, katika mkutano wa kwanza uliohusisha Mawaziri wa uchukuzi kutoka nchi ya Tanzania, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mkutano huo umejadili ushirikiano katika miradi ya maendeleo ya pamoja baina ya nchi hizo.[/caption]

“Kukamilika kwa reli ya Kati ya kisasa hadi Uvinza- Msongati kutawezesha reli hiyo kuunganisha vizuri nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi na hivyo kuchochea maendeleo katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika”, amesisitiza Waziri wa Uchukuzi wa Burundi, Eng. Jean Bosco Ntunzwenimana.

Mawaziri hao wameelezea umuhimu wa uboreshaji wa huduma za uchukuzi katika Bandari ya Ziwa Tanganyika ili iwe na viwango vya kimataifa na kuunganisha vizuri ukanda huo.

Mkutano huo ni mkakati wa nchi za Ukanda wa Ziwa Tanganyika wenye lengo la kuboresha huduma za usafirishaji na uchukuzi katika nchi hizo ili kukuza uchumi na kurahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi