Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, ameizindua rasmi Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, ambayo itakuwa ikishughulikia masuala ya taaluma ya waandishi wa habari
Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 03, 2025 Jijini Dar es Salaam, ambapo imehudhuriwa na wadau wa habari, waandishi wa habari, pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya habari nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kabudi amesema kuzinduliwa kwa bodi hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha weledi wa taaluma ya uandishi wa habari, kuchochea uwajibikaji na kulinda haki za waandishi wa habari.
“Leo ni siku ya kihstoria, tunapoizindua bodi ya ithibati ya waandishi wa habari, iliyozuiliwa kwa muda wa miaka nane, tangu ilipoundwa chini ya sheria ya huduma za habari sura ya 229 ya sheria za Tanzania, ikiwa na lengo la kuimarisha weledi, uwajibikaji na heshima ya taaluma ya habari hapa nchini” amesema Profesa Kabudi
Amesema bodi hiyo ni chombo muhimu katika kusimamia viwango vya taaluma ya uandishi wa habari, kuhakikisha uzingatiaji wa maadili ya kitaaluma, pamoja na kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuboresha weledi wao.
Katika Uzinduzi huo Waziri Kabudi pia amemkabidhi zana za Kazi Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Tido Mhando, zinazojumuisha Sera ya Habari, Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni zake.
Miongoni mwa majukumu ya Bodi hiyo yanayotarajiwa kuanza kutekelezwa mapema mara baada ya kuzinduliwa ni pamoja na kutoa Ithibati na Vitambulisho (Press Card) kwa Waandishi wa Habari waliokidhi vigezo vilivyoainishwa kisheria na kusimamia maadili ya taaluma ya Uandishi wa Habari.
Kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imepewa mamlaka ya kutoa Vitambulisho kwa Waandishi wote kutoka vyombo vya habari vya umma, binafsi, pamoja na waandishi wa kujitegemea.
Awali, utoaji wa vitambulisho hivyo kwa Waandishi wa Habari ulikuwa ukifanywa na Idara ya Habari-MAELEZO kabla Bodi ya Ithibati kuundwa na kuanza majukumu yake rasmi.
Bodi hiyo ilitangazwa Septemba 18 mwaka jana baada ya Waziri mwenye dhamana kumteua Bw. Mhando na wajumbe wengine sita kuunda bodi hiyo, sanjari na kuwahamishia watumishi sita kutoka wizarani kuunda Sekretarieti ya bodi hiyo.