Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ameielekeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari nchini kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wote wanazingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia taaluma yao.
Amesema ithibati ya wanahabari itasaidia kudhibiti uandishi usio wa kimaadili na kuongeza heshima ya taaluma hiyo.
Ameyasema hayo leo Machi 3, 2025 wakati akizindua bodi ya ithibati ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa bodi hiyo inapaswa kuanza kwa kuwalea na kuwapa miongozo mbalimbali juu ya taaluma yao.
“Bodi inapaswa kuandaa na kusimamia utaratibu wa usajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma, mfumo huu unapaswa kuwa shirikishi na unaoendana na maendeleo ya teknolojia na mazingira ya sasa ya sekta ya habari” amesema Profesa Kabudi.
Aidha, Profesa amesema kuwa, bodi ina jukumu la kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma kwa kutoa miongozo na mafunzo ya mara kwa mara, pia, ni muhimu kuwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko na ukiukwaji wa maadili kwa haki na uwazi.
Aidha amesema, ili kufanikisha majukumu yake, bodi inapaswa kushirikiana na vyombo vya habari, vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari, na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanapata mafunzo ya mara kwa mara na kuwa na ujuzi wa kisasa.
“Wananchi wanapaswa kuelewa umuhimu wa ithibati ya waandishi wa habari na jinsi inavyosaidia kuboresha sekta ya habari. Bodi inapaswa kuandaa programu za uelimishaji ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa taaluma hii kusimamiwa ipasavyo, katika ulimwengu wa sasa wa kidijiti, bodi hii inapaswa kusaidia kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanatumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili” amesema Profesa Kabudi.
Ameongeza kuwa, ni muhimu pia kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika utoaji wa habari huku akiendelea kuiagiza bodi hiyo kushirikiana na mamlaka husika, kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa usalama bila vitisho, unyanyasaji au vikwazo visivyo vya lazima. Usalama wa wanahabari ni msingi wa uhuru wa vyombo vya habari.