Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Watu wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha ukomavu wa kisiasa kupitia dhamira yake ya kuhimiza maridhiano ya kitaifa kwa kushirikisha vyama vya siasa.
Prof. Kabudi amesema hayo Oktoba 7, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizindua uongozi mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa pamoja na nembo mpya ya Baraza hilo.

Amesema Rais Samia amekuwa msikivu na mwenye utulivu katika kusikiliza maoni ya wananchi na wadau mbalimbali, akilenga kuimarisha umoja, mshikamano na amani nchini.
“Rais Samia amekuwa na dhamira ya dhati ya kuanzisha 4R, ambazo zimeonekana kuwa na matokeo chanya katika kuleta nchi pamoja na kuondoa tofauti zetu. Amekuwa na utulivu wa kumsikiliza kila mtu ambaye amewahi kukutana naye,” amesema Prof. Kabudi.
Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa Baraza hilo kunapaswa kuwa chachu kwa viongozi wake kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Aidha, Prof. Kabudi amewataka viongozi wapya wa Baraza hilo kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa kanuni za Baraza, ikiwemo kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake na wadau wengine katika mijadala na shughuli zake.
Amesema Baraza hilo ni jukwaa muhimu la kujadili changamoto mbalimbali za kisiasa, ikiwemo zile zinazoonekana kuwa ngumu kutatuliwa, huku akiwataka viongozi kulitumia jukwaa hilo kujenga maelewano na mshikamano wa kitaifa.
Prof. Kabudi pia amesisitiza umuhimu wa kutumia misingi ya 4R kama dira ya kuimarisha ushirikiano na kupiga hatua katika masuala mbalimbali ya kisiasa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Juma Ally Khatib, amesema Baraza hilo litaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kwa lengo la kuchochea maendeleo na kujenga mazingira chanya ya kisiasa nchini.

Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Eveline Munishi, amesema uwepo wa Baraza hilo utasaidia kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini.
Mkutano huo umeandaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi. Baraza hilo la Vyama vya Siasa lilichaguliwa Septemba 3, 2026, na linatarajiwa kudumu madarakani hadi Septemba 3, 2028.
Kwa sasa, Baraza hilo linaongozwa na Mheshimiwa Juma Ally Khatib ambaye ni Mwenyekiti, huku Mheshimiwa Aggrey Mwanri akiwa Makamu Mwenyekiti.