Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Prof. Mbarawa: Fidia Zitalipwa kwa Wanaostahili Kisheria
Jul 18, 2017
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akipokea taarifa kutoka kwa Mkandarasi wa Kampuni ya CHICO (katikati), anayejenga barabara ya Mwigumbi-Maswa KM 50.3 inayojegwa kwa kiwango cha lami ambao ujenzi wake umefikia takribani asilimia 77.

Na. Mwandishi Wetu

Serikali imesema itawalipa fidia kwa mujibu wa sheria wananchi wote waliopisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati akizungumza na wananchi wa Mwigumbi mkoani Shinyanga alipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi - Maswa yenye urefu wa Kilometa 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa Kampuni ya CHICO kwa gharama ya  kiasi cha Shilingi Bilioni 61.

"Kila anayestahili kulipwa fidia atalipwa kama Sheria inavyoelekeza na endapo akatokea yeyote mwenye malalamiko Serikali ipo itamsikiliza", alisema Waziri Prof. Mbarawa.

Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.135 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Mwanza.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi na Viongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wa Mkoa ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na spidi inayotakiwa.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa aliwahimiza makandarasi wote nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa maeneo husika inapopita miradi ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuwapatia kipato na kuinua uchumi wao.

Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Batholomeo Ndirimbi, alisema mpaka sasa tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya ulipaji fidia na watahakikisha kuwa fedha hizo zinalipwa kwa watu sahihi wanaostahili fidia.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mwigumbi, wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa KM 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

"Tutasimamia zoezi hili kwa umakini na kutoa fidia kwa wale wote wanaostahili kisheria", alisema Mhandisi Ndirimbi.

Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 77 ya ujenzi na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa alikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa Kilometa 16.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75 na daraja la Nyashishi lenye urefu wa mita 67.9 ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.5 mkoani Mwanza.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza Mhandisi Marwa Rubirya, alisema ujenzi wa barabara hiyo unaendelea vizuri na mkandarasi atamaliza kwa wakati uliopangwa na viwango walivyokubaliana katika mkataba.

Aliongeza kuwa barabara hiyo inapita katika Wilaya mbili ambazo ni Misungwi na Magu na kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo katika wilaya hizo na mikoa jirani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi