Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Prof. Mbarawa Awataka TBA Kumaliza Nyumba ya Jaji Mfawidhi
Jul 17, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha ndani ya miezi sita wanakamilisha ujenzi wa nyumba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani humo wakati alipokagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala huo ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa kuwapatia waheshimiwa majaji mahali pazuri pa kuishi ili waweze kutimiza wajibu wao wa kutenda haki kwa wananchi ipasavyo.

“Hakikisheni mnakamilisha ujenzi wa nyumba hii haraka iwezekanavyo ili Mheshimiwa huyu apate mahali pazuri pa kuishi, kufanya hivi kutarahisisha majukumu yake na kufanikish utendaji wa kazi”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Amesisitiza umuhimu wa Wakala huo kuongeza kasi katika miradi mbalimbali inayoendelea ya ujenzi wa nyumba za viongozi ili kuondoa adha ya kodi za pango kubwa zinazopotea kwa viongozi hao kupanga kwa watu binafsi.

Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga Mhe. Jaji Richard Kibella amemshukuru Prof. Mbarawa kwa niaba ya taasisi zake za TBA na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kwa namna ambavyo wameshirikiana na Mahakama kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na kuwapatia huduma nyingine za uendeshaji.

Aidha, ameiomba Serikali kukamilisha kwa haraka ujenzi wa nyumba za viongozi na watumishi wa Mahakama kwani gharama kubwa zinatumika katika malipo ya upangaji wa nyumba za viongozi.

“Mhe. Prof. Mbarawa suala la nyumba ni changamoto, nyumba za kupanga zina gharama kubwa ambapo kwa namna moja au nyingine inaongeza gharama za uendeshaji wa Mahakama na kupunguza usalama”, amefafanua Jaji Kibella.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama hiyo Bwana Ernest Masanja, amemueleza Prof. Mbarawa kuwa kukamilka kwa jengo la Mahakama hiyo kumewezesha Majaji na watendaji wengine wa Mahakama kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na kwa wakati katika kuwapatia Wananchi haki.

Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Mkoa huo unaosimamiwa na TBA na ameuelekeza Wakala huo kushirikiana na Mamlaka husika kuhakikisha kuwa ujenzi wake unazingatia viwango na ubora na kukamilika kwa wakati.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi