Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Posta Tanzania na Oman Zaingia Makubaliano 17 ya Ushirikiano Kiuchumi Kupitia Utumaji wa Vifurushi
May 31, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Grace Semfuko, MAELEZO.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameshuhudia utiaji saini makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Posta la Tanzania na Shirika la Posta la nchini Oman ambayo yanalenga kuimarisha mahusiano na kukuza uchumi kwa nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yaliyopo kwenye maeneo 17 ya ushirikiano ni pamoja na uunganishwaji wa maduka mtandao, uchapishaji wa stempu ya pamoja na kubadilishana ujuzi na teknolojia ya utoaji wa huduma za posta kwa wananchi ikiwemo ya usafirishaji wa barua, nyaraka, vifurushi, mizigo na sampuli za maabara, huduma za utumaji wa fedha na uwakala, biashara ya kuuza na kununua fedha za kigeni, biashara za mtandao na huduma nyinginezo zinazotolewa na posta.

Postamasta Mkuu wa Tanzania, Bw. Macrice Mbodo na Mtendaji Mkuu wa Posta ya Oman, Bw. Nasser Ahmed Nasser Al Sharji ndio waliotia saini makubaliano hayo mbele ya Waziri Nape.

"Mmechukua uamuzi mzuri sana za kupanua huduma ndani na nje ya nchi yetu, hizi ni jitihada za hali ya juu kwa kuzingatia mkazo wa Serikali ya Awamu ya Sita ya hapa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifungua Tanzania Kimataifa, kurudisha na kuimarisha mahusiano ya kimataifa kwa njia za kidiplomasia na kibiashara, hivyo hatua hii inaonesha jinsi ambapo Posta Tanzania inavyokwenda sambamba na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais.” Amesema Mhe. Nape.

Amesema huduma za posta zimekuwa ni kiungo kizuri cha mawasiliano tangu enzi na enzi ambapo huduma za mwanzo za ustaarabu wa mawasiliano zilikuwepo na kuongeza kuwa huduma hizi zimekuwa zikibadilika kadri mwanadamu anavyozidi kukua kifikra, kiteknolojia na kiuchumi ambapo pamoja na mabadiliko haya mpaka hivi leo, sekta ya posta bado ina umuhimu mkubwa kwa jamii kwenye mataifa mbalimbali.

"Ushirikiano huu ni wa manufaa kwa pande zote mbili, manufaa hayo hayaishii kwenye hizi taasisi mbili tu, bali unaenda hadi kwenye Serikali zetu zote, kwa pamoja tunapata zaidi na kupitia ushirikiano huu ni matumaini yangu kwamba tutaimarisha na kuona kwa namna ambavyo kwa pamoja tutaimarika.” Amesema Mhe. Nape.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo amesema mageuzi ya kiutendaji ya kuifanya Posta ya Tanzania kuwa Posta ya Kidigitali na yanayoendelea kufanywa na Serikali, yanaipa heshima kubwa Posta ya Tanzania na Taifa kiasi cha kuyavutia mashirika mengine ya posta kuja kujifunza na kushirikiana.

"Leo hii tukiwa na Posta ya Oman mazungumzo na posta nyingine yanaendelea ikiwepo posta ya Dubai, Posta ya Kenya, Posta ya Burundi, Posta ya Zimbabwe, na nchi nyinginezo, hii ni kutokana na jitihada kubwa za Serikali, hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Posta Tanzania na Posta Oman ina maeneo 17 ya ushirikiano ambayo si tu yanalenga kuboresha utendaji kazi wa mashirika hayo, lakini pia yanalenga kupanua wigo na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za mashirika haya kwa wananchi wa Tanzania, Oman na kwingineko Duniani”, amesema Bw. Mbogo.

Nae Mtendaji Mkuu wa Posta Oman, Bw. Nasser Ahmed Nasser Al Sharji amesema mageuzi ya utendaji yanayofanywa na yanayoendelea kufanywa na Shirika la Posta Tanzania yameipa heshima posta ya Tanzania kimataifa, na ndio maana Oman imeona fursa ya kushirikiana.

"Mimi na bila shaka Watendaji Wakuu wa posta za nchi nyingine duniani tuna imani kubwa na utendaji kazi wa Bw. Macrice Mbodo na tunatarajia mafanikio makubwa zaidi kwa posta ya Tanzania na mashirikiano yake na posta zingine, Posta ya Oman tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wowote unapohitajika kufanya hivyo”, amesema Bw. Nasser Al Sharji.

Amesema kutokana na maboresho ya kidigitali yanayofanywa na yanaoendelea kufanywa na taasisi hizi mbili ili kukidhi mabadiliko ya teknolojia yanaoendelea duniani, wameona ni vyema kushirikiana ili kila mmoja afaidike na fursa zilizopo kwa mwingine.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi