Na: Lilian Lundo
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa mafunzo ya uandishi wa habari za kitakwimu kwa wanachama wa chama cha waandishi wa habari Dodoma ili kuwaongezea uwezo wa uandishi mzuri wa habari za kitakwimu.
Mafunzo hayo ya siku mbili kuanzia tarehe 26 hadi 27 Mei, mwaka huu yanayofanyika katika ukumbi wa Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Jijini Dodoma yamefunguliwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara hiyo.
Akifungua mafunzo hayo Zamaradi Kawawa amesema kutokana na Wizara zote pamoja na baadhi ya Taasisi kuhamia Dodoma, Dodoma imekuwa ndio kitovu cha shughuli za Serikali kwa maana hiyo imekuwa chanzo kikuu cha habari zinazohusu Serikaki nchini hivyo basi majukumu ya vyombo vya habari vilivyopo mkoani Dodoma yameongezeka na yatazidi kuongezeka kadiri shughuli za Kiserikali zinavyoongezeka.
"Hapana shaka yeyote kuwa watumishi wote wa vyombo vya habari vilivyopo Dodoma wanahitaji mafunzo kama haya kwa ajili ya kuimarisha weledi wao katika kuripoti matukio mbalimbali yanayotokea mkoani humu," amesema Zamaradi.
Aidha amesema, maisha ya kila siku ya mwanadamu yanahusishwa na takwimu hivyo takwimu ni sehemu muhimu ya maisha ya ulimwengu wa sasa na ndizo zinazotawala namna ya kufikiri na kufanya maamuzi katika maisha tunayoyaishi.
Ametolea mfano wa ubora wa maisha ya watu kuwa unapimwa kwa kutumia takwimu, hali ya uchumi, hali ya biashara, uwekezaji, huduma za usafiri na usafirishaji na hata michezo. Hivyo basi, uandishi wa habari hauwezi kukwepa matumizi ya takwimu.
Hata hivyo ametoa wito kwa NBS kuendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoani ambakk hivi sasa kuna redio nyingi za kijamii ambazo zinasikilizwa na Watanzania wengi. Waandishi wa redio hizo wakipata ujuzi wa uandishi wa habari za kitakwimu itasaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Kwa upande wake, Meneja wa Takwimu za Kodi wa NBS Fred Matola amesema matarajio ya NBS baada ya mafunzo hayo ni kuwa na waandishi wa habari mahiri kwa Jiji la Dodoma kwa ajili ya kuhabarisha Umma.
"Mafunzo haya yatakuwa tija kwa waandishi wa Dodoma hivyo kuwanufaisha Watanzania wote kupitia habari watakazoandika," amesema Matola.
Naye, Mratibu wa Mafunzo hayo Said Ameir amesema mafunzo hayo ni ya kipekee, kutokana na Serikali kuhamia Dodoma na shughuli nyingi za Serikali kufanyika mkoani humo. Mafunzo hayo ni ya Siku mbili yanashirikisha waandishi wa habari zaidi ya arobaini kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari.