Na Rhoda James, Geita
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameutaka Mgodi wa Geita Gold Mine Ltd kuwalipa fidia wananchi waliopata madhara ya nyufa katika katika nyumba zao kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini wa kampuni hiyo.
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo tarehe 26 Septemba, 2018 wakati alipofungua Maonesho ya Kwanza ya Teknolojia ya Uchimbaji na Uwekezaji wa Madini ya Dhahabu mkoani Geita kwa niaba ya Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
Alitoa rai kwa Wachimbaji wadogo wa madini kote nchini kushiriki maonesho hayo yanayoendelea mkoani humo kwa kuwa yatawanufaisha kwa kupata fursa ya kujifunza kuhusu teknolojia mbalimbali na namna bora ya uchimbaji, uchenjuaji, ikiwemo kupata elimu ya kulinda mazingira na kuzalisha kwa tija.
Pia, aliwataka Wakuu wa mikoa yote nchini pamoja na Wakuu wa wilaya zote kujifunza kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Gabriel Luhumbi ili kuhakikisha kuwa wananchi wao wanafaidika na rasilimali pamoja na mazao yanayolimwa katika maeneo yao.
“Mkifanya maonesho ya aina hii katika mikoa yenu kulingana na mazao au rasilimali mlizonazo katika mikoa yenu wananchi wenu watafaidika,” alisema Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo.
Vilevile, Naibu Waziri Nyongo, aliwataka wananchi wa mkoa wa Geita na Kagera pamoja na wadau wa madini ya dhahabu kujipanga ili kuhakikisha kuwa maonesho hayo yanafanyika kila mwaka.
Pia, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana na uongozi kutoka Mkoa wa Geita kuhakikisha kuwa wanayatangaza maonesho hayo kwa kiasi kikubwa ili yaweze kufahamika duniani kote hatimaye wadau wa madini waweze washiriki kwa wingi.
“Wateja wengi wa madini wanatoka nje ya nchi na ni vyema pia wakajua chanjo cha madini hayo kiko wapi,” alisema Nyongo.
Akizungumzia mchango wa Sekta ya madini katika pato la taifa, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, mchango wa Sekta ya Madini bado ni kidogo na kuongeza kuwa, malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa, mchango wake unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
“Mwaka 2016 na 2017 sekta ya madini imechangia kwenye pato la taifa asilimia 4.8 lakini tunatarajia ifikapo 2025 sekta ya madini itachangia zaidi ya asilimia10,” alisema Nyongo.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Nyongo ametoa onyo kwa wachimbaji wadogo kuachana na tabia ya kutorosha madini na kueleza kuwa, atakayekamatwa akifanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia, Naibu Waziri Nyongo alitumia fursa hiyo kuupongeza Mkoa wa Geita na wadau mbalimbali akiwemo Mamlaka ya Maendeleo ya Bishara Tanzania (TanTrade) pamoja na Wizara ya Madini kwa kuandaa maonesho ya madini ya dhahabu mkoani Geita.
Pia, amewapongeza umoja wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya dhahabu (GEREMA) kwa kuhakikisha kuwa Maonesho hayo yanafanyika kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Gabriel Luhumbi alisema kuwa, ni matarajio yake kuwa maonesho hayo yatakuwa ya kitaifa na hatimaye ya dunia nzima na kuongeza kuwa, anataka maonesho hayo ya madini ya dhahabu kufanyika kila mwaka mkoani kwake.
Pia, alisema alitumia fursa hiyo kuishukuru Wizara ya madini kwa ushirikiano inayotoa kwa wachimbaji wadogo kupitia taasisi za GST na STAMICO.