Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema takribani nusu ya maisha ya Hayati Edward Lowassa yametumika katika utumishi wa uongozi wa umma na kwamba amejitolea muda na maisha yake kwa ajili ya nchi yake na kubeba dhamana ya uongozi.
Amebainisha hayo leo Monduli wakati akiongoza maelfu ya waombolezaji kwenye maziko ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa huku akisisitiza kuwa aliweza kuacha alama kubwa na za kudumu katika kila jukumu lililomkabili.
"Hayati Edward Lowassa alikuwa na mapenzi makubwa si kwa familia yake tu bali kwa watu wote ikiwemo taifa letu la Tanzania, ametuachia mafunzo matatu makubwa ambayo ni ushupavu, ustahimilivu na ulezi," alisema Dkt. Samia.
Alisisitiza kuwa Hayati Edward Lowassa alikuwa kiongozi jasiri na shupavu, alisimamia masuala mbalimbali ya serikali na chama bila kuyumba, anakumbukwa kwa kuishauri vema Serikali kuhusu matumizi ya maji ya Ziwa Victoria licha ya shinikizo kubwa lililokuwepo la kutotumia maji hayo kwa sababu za kihistoria ambapo hadi sasa maji hayo yanatumika vyema kwenye mikoa ya Shinyanga na Tabora vilevile Serikali imeshaamua maji hayo kufika katika mikoa ya Singida na Dodoma.
"Ndugu yetu Hayati Edward Lowassa alikuwa na sifa ya ulezi, amewalea vijana wengi wakati wa uongozi wake ambao ni viongozi wetu wa sasa, msingi huu wa malezi ulidhihirika hasa mwaka 2015 alipokuwa akigombea urais ambapo alipambanua vipaumbele vyake vikuu vitatu kuwa cha kwanza ni Elimu, cha pili Elimu na cha tatu Elimu, hii ilionesha wazi kwamba anapenda vijana wapate maarifa na ujuzi kwa ajili ya familia zao na maisha yao kwa ujumla," aliongeza Rais Samia.
Hayati Edward Lowassa ni mwanzilishi wa shule za sekondari za kata ambapo akiwa Waziri Mkuu alisimamia na kuratibu ujenzi wa shule za sekondari kila kata nchini ili kuongeza idadi ya wanafunzi kwenye elimu ya sekondari, sera hii inaendelezwa na serikali hadi leo kwani tuna idadi ya shule za sekondari za kata zaidi ya 5,000 kutoka shule 828 mwaka 2004
Rais Samia amezidi kumuelezea Hayati Edward Lowassa kuwa alipofanya maamuzi ya kuhamia chama kingine aliendelea kunadi sera zake bila kumtukana, kumkejeli wala kumzushia mtu yeyote, na aliporudi Cha Cha Mapinduzi (CCM) hakuwahi kuwananga, kuwazodoa, kuwakebehi wala kuwasema vibaya wapinzani. Hapa tunapata somo kubwa la siasa za kujenga hoja, kuheshimiana, kustahimiliana na siasa za keleta maendeleo, huo ni ukomavu mkubwa wa kisiasa.
"Tunapaswa kumuenzi Hayati Edward Lowassa kwa kuliweka taifa mbele zaidi ya itikadi za vyama vyetu ili taifa letu liendelee kubaki salama kwa kufanya siasa za kistaarabu kwa kuyaweka maslahi ya nchi mbele kwa kujadili masuala mbalimbali kwa hoja," alisema Mkuu wa Nchi.
Historia ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa hapa duniani imetamatika leo baada ya maziko yake kijijini Ngarash, wilayani Monduli, mkoani Arusha.