Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NSSF Kuboresha Kima cha Chini Pensheni ya Mwezi Kufikia 150,000
Mar 17, 2025
NSSF Kuboresha Kima cha Chini Pensheni ya Mwezi Kufikia 150,000
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 17, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) upo kwenye hatua za mwisho za kuboresha kiwango cha kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000 ikiwa ni moja ya maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bw. Masha Mshomba amesema hayo leo Machi 17, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mfuko huo ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Pamoja na maboresho hayo ya kiwango cha kima cha chini cha pensheni, viwango vingine vya pensheni vinatarajiwa pia kuongezeka kwa kati ya asilimia 2 na asilimia 20 ambapo utekelezaji wake utaanza mara moja baada ya taratibu za uidhinishwaji kukamilika, utahusisha kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari 2025”, amesema Bw. Mshomba.
.
Ameongeza kuwa, kutokana na utendaji mzuri wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwajali wastaafu, Mfuko umeendelea kuboresha tena ulipaji wa mafao kwa wanachama wote waliokuwa wanalipwa mkupuo wa awali wa asilimia 33 na kuanzia mwezi Julai 2022, waliongezewa kiwango cha mkupuo kufikia asilimia 35.

Katika hatua nyingine Bw. Mshomba ameeleza kuwa, Mfuko huo ulilipa mafao ya shilingi trilioni 3.11 ambapo malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69 kutoka shilingi bilioni 537.08 katika mwaka ulioishia wa Februari 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 909.16 katika mwaka ulioishia Februari 2025.

Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, thamani ya Mfuko huo imeongezeka kwa asilimia 92 kutoka shilingi trilioni 4.8 mwezi Februari 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 9.2 mwezi Februari 2025. Ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, mapato yatokanayo na michango na kukua kwa thamani ya vitega uchumi vya Mfuko.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi