Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NIT: Mafunzo ya Urubani Nchini Muarobaini Gharama za Nje
Mar 20, 2025
NIT: Mafunzo ya Urubani Nchini Muarobaini Gharama za Nje
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa chuo hicho katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 20, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Adelina Johnbosco - MAELEZO

Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kinachoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Dkt.  Samia Suluhu Hassan, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kimeanzisha kozi mpya ya urubani yanayotarajiwa kuanza mwezi Mei 2025.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo hicho, Mhandisi, Dkt. Prosper Mgaya wakati akieleza mafanikio na mwelekeo wa chuo hicho ndani ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, leo Machi 20, 2025 katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.

"Serikali ya Awamu ya Sita imekiwezesha Chuo cha NIT kukamilisha maandalizi ya utoaji wa mafunzo ya Urubani ambapo Chuo tayari kimekamilisha matakwa ya kupata ithibati kutoka TCAA kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo, na katika kukiwezesha Chuo kuanza mafunzo haya Serikali imetoa shilingi takribani bil. 6 kwa ajili ya uwezeshaji" amesema Mha. Dkt. Mgaya

Vile vile, amefafanua jinsi ilivyokuwa gharama kubwa wahitaji wa kozi hii walipoifuata kwenye nchi za nje.

"Kama nchi tumekuwa tukitegemea kwa kiasi kikubwa kupelekea Watanzania kupata mafunzo ya urubani nje ya nchi. Hivyo Serikali na watanzania kwa ujumla tumekuwa tukitumia fedha nyingi sana za kigeni kusomesha marubani nje ya nchi. Kwa kuanzisha mafunzo haya hapa nchini kwenye Chuo cha Umma (NIT) kutapunguza gharama ya mafunzo kwa takribani asilimia 50 - 60 ambazo watanzania wengi wanatumia kupata mafunzo hayo nje ya nchi" ameongeza Mha. Dkt. Mgaya

Aidha, amesema kuanza kwa mafunzo haya kutaongeza idadi ya marubani wazawa hapa nchini hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa marubani wa kigeni ambao gharama yake ni kubwa.

"Katika kuhakikisha Chuo kinaanza mafunzo ya Urubani, Serikali imegharamia mafunzo ya wakufunzi watano ambao wamepata mafunzo haya nchini Afrika ya Kusini kwa gharama ya shilingi bil. 1.5 ikiwa ni wastani wa shilingi milioni 300 kwa kila mkufunzi" - Mha. Dkt. Mgaya

Kwa mujibu wa Mha, Dkt. Mgaya amesema, katika kuhakikisha kwamba Serikali imejidhatiti katika hilo, tayari imenunua ndege mbili za mafunzo  aina ya Cesna 172 zenye injini moja ambazo tayari zipo nchini kwa ajili ya kuanza kutumika katika kutoa mafunzo zikiwa na thamani ya shilingi bil. 2.9 huku ndege nyingine tatu, moja  ikiwa ya injini mbili yenye thamani ya shilingi bil. 5.9 ambayo itawasili Oktoba 2025 na mbili za injini moja zinatarajiwa kuwasili nchini mwaka 2026.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi