Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NIC Yatoa Bilioni 1.7 Gawiwo kwa Serikali.
Jun 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_3142" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga akimkabidhi Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), hundi kifani yenye thamani ya Sh. bil. 1,7 ambazo ni gawiwo ambalo Serikali imepata baada ya Shirika hilo kupata faida kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Tukio hilo lilifanyika leo Makao Makuu ya Wizara Mjini Dodoma.[/caption]

Na Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma

SERIKALI imeendelea kupata neema kutokana na uwekezaji wake kwenye mashirika na taasisi mbalimbali yanayojiendesha kibiashara nchini ambapo leo Shirika la Bima la Taifa (NIC) limetoa gawiwo la Shilingi bilioni 1.707 baada ya kupata faida kiabishara mwaka 2016/2017.

Kwa nyakati tofauti mwaka huu, Serikali ilipokea kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kufuatiwa na NMB Bank Plc, iliyotoa kiasi cha Shilingi bilioni 16.5 hivi karibuni.

Akipokea Hundi kifani ya kiasi hicho cha Shilingi 1.707 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa, Bw. Sam Kamanga, Waziri wa Fedha na Mipango, amelipongeza shirika hilo kwa kuonesha maendeleo makubwa katika kipindi kifupi tangu azindue Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo mwishoni mwa mwaka uliopita.

[caption id="attachment_3145" align="aligncenter" width="750"] Viongozi waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango, wakishiriki tukio la Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuikabidhi Serikali gawiwo la Sh. Bil. 1.7 baada ya Shirika hilo kufanya vizuri kibiashara katika Mwaka wa Fedha 2016/2017. Tukio hilo lilifanyika leo makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, mjini Dodoma.[/caption]

“Nilipozindua Bodi yenu ya Wakurugenzi uliniahidi Mkurugenzi Mtendaji kuwa mtafanyakazi kwa bidii na kuanza kutoa gawiwo Serikalini, ninajisikia furaha sana kwa niaba ya watanzania kuona kuwa mnatimiza ahadi hiyo kwa kutoa asilimia 15 ya pato ghafi la mapato yenu. Nawapongezeni sana” alisisitiza Dkt. Mpango.

Alizitaka taasisi nyingine za umma zilizochini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina zinazofikia 260 kuanza kutumia huduma za bima kupitia Shirika la Bima la Taifa.

Alisema anafahamu kwamba kuna taasisi nyingine zina mikataba na mashirika mengine ya bima lakini akatoa wito kwa taasisi hizo kwamba baada ya kumaliza mikataba yao, waanze kupata huduma kupitia NIC ambalo manufaa yake yameanza kuonekana baada ya kuanza kurejesha sehemu ya faida yake kwa Serikali.

Hata hivyo Dkt. Mpango aliitaka NIC lisibweteke badala yake liboreshe huduma zake ili kuweza kujiongezea soko kwani mashirika ya bima yamekuwa na ushindani mkubwa.

Alilitaka Shirika hilo kutoa elimu kwa Umma wakiwemo wakulima, wafugaji na wananchi wengine kuhusu umuhimu wa kukatia bima mifugo, mazao, nyumba na vyombo vya moto ili kujiepusha na hasara zinazoweza kutokea wakati wa majanga.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alisema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kwa Shirika hilo kutoa gawiwo kwa Serikali tangu lianzishwe miaka 54 iliyopita na kuzitaka Taasisi zote zilizo chini ya Wizara kuiga mfano wa NIC.

[caption id="attachment_3148" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, akitoa neno la Shukrani kwa uongozi Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa ubunifu na uwajibikaji wao ulioliwezesha Shirika hilo kupata faida na kutoa gawiwo kwa Serikali. Tukio hilo lilifanyika leo makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, mjini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango.[/caption]

“Naamini leo ndiyo mmezaliwa na mna miaka mingine 100 mbele ya kutenda kwa ajili ya watanzania” Alisisitiza Dkt. KIjaji

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Dotto James alilipongeza Shirika hilo na kusisitiza kuwa Wizara ipo bega kwa bega kushirikiana nao ili kuhakikisha Shirika hilo linapiga hatua zaidi kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi kifani, Mkurugenzi Mtendaji wa  Shirika  la Bima ya Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuzihamasisha Taasisi za Umma kukata bima NIC, na kwamba hatua hiyo ndiyo imeliwezesha shirika kutengeneza faida na kutoa gawiwo kwa Serikali.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuyahamasisha mashirika zaidi ya 200 yaliyochini ya Msajili wa Hazina kutumia huduma za Taasisi yake ili kuongeza wigo wa mapato na kuleta faida zaidi kwa wabia wa Shirika hilo

“Ni Taasisi 15 tu ndizo zilizoitikia wito wa Serikali wa kutumia huduma za bima kupitia NIC lakini mashirika na taasisi nyingine bado hivyo ninaiomba Serikali itusaidie kufanikisha jambo hili” Alisistiza Bw. Kamanga.

Aliiahidi Serikali kwamba Shirika lake linatarajia kuongeza gawiwo zaidi za kiasi hicho kilichotolewa kutokana na mikakati kabambe ya kiabiashara waliyojiwekea.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi