Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NHIF Watakiwa Kuongeza Wanachama.
Aug 21, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na.Mwandishi Wetu -Rukwa

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetakiwa kuongeza jitahada za kuwasajili wanachama wapya ili kuviwezesha vituo vya Afya serikali   kutoa huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Afya,maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati alipotembelea kituo cha afya cha Mazwi kilichopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Alisema Mkoa wa Rukwa umefikia asilimia 27 ya wananchi wanaotumia bima ya afya Kitaifa,hivyo waongeze kuwashawishi wananchi wengi zaidi kujiunga na mfuko huo pamoja na mfuko wa afya ya Jamii(CHF).

“Nimesema kuanzia sasa ninaanza kuwapima kwa kusajili wananchi ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa ajira,ninataka vijana wengi wajiunge kwa wingi kwa kujiunga kama kikundi na kujiunga na bima inayojulikana kama  ‘Kikoa” ambayo kujiunga kwake ni kuanzia watu kumi’’ alisisitiza Waziri Ummy.

Kuhusu Mfuko wa Afya ya jamii(CHF) Waziri alisema kwa sasa kuna CHF iliyoboreshwa hivyo kadi hiyo inatumika kwenye vituo vyote vya halmashauri  na si pale mwanachama alipokatia,”ni bora tuwachangishe elfu kumi kumi za watanzania ili tuweze kufikia usajili wananchi wengi na kupata huduma za afya bila vikwazo’’ alisema.

Waziri Ummy aliishauri Manispaa hiyo kutengezea kadi ambayo itakua rafiki kwa mwanachama kuweza kuiweka kwenye pochi au mahali pengine ambayo itakua rahisi kwa kutunza tofauti na kadi ya hivi sasa ambayo ni kubwa.

Aidha,alisema Wizara yake inampango wa kuongeza gharama ya CHF iliyoboreshwa ya  shilingi elfu ishirini ili mwenye kadi hiyo aweze kupata huduma hadi katika hospitali ya Mkoa.

“ Tunataka kila mtu apate huduma za tiba bila kikwazo, leo una hela, kesho huna na una umwa bora utoe elfu kumi ya CHF utibiwe ndani ya Manispaa tena siyo peke yako bali na watu wako watano,alisema Waziri Ummy.

Waziri alipiga  marufuku  kwa mtu mwenye kadi ya CHF anapoenda kwenye vituo vya huduma ya afya kuambiwa akanunue kipimo au dawa bali wanatakiwa kupata vipimo vyote.

Mwisho.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi