Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NHIF Ina Ziada ya Shilingi Bilioni 95 - Dkt. Irene
Mar 10, 2025
NHIF Ina Ziada ya Shilingi Bilioni 95 - Dkt. Irene
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 10, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kufanya jitihada mbalimbali za kuboresha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hadi kufikia Disemba 2024, mfuko una ziada ya shilingi bilioni 95 huku ukiondoka kwenye nakisi ya zaidi ya shilingi bilioni 120.

Dkt. Irene Isaka amesema hayo leo Machi 10, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mfuko huo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni programu inayoratibiwa na Idara ya Habari - MAELEZO.

Dkt. Irene amesema ziada hiyo imepatikana baada ya kuondoa mianya mbalimbali ikiwemo kukabiliana na udanganyifu, watumishi wa NHIF kujituma na kubana matumizi. Aidha, kutokana na kuongezeka kwa ziada hiyo, malipo kwenda kwenye vituo vya afya yanalipwa kwa wakati.

"Katika kipindi cha nyuma, mfuko ulitetereka, ulikuwa na uwezo wa kujiendesha kwa kipindi cha miezi sita tu lakini kwa sasa mfuko umeboreka na kuwa na uwezo wa kujiendesha kwa mwaka mmoja na miezi miwili, lengo la NHIF ni kufikisha uwezo wa kujiendesha kwa miaka miwili", amesema Dkt. Irene.

Pia, Mfuko ulikuwa na uwiano wa madai wa asilimia 132 lakini kwa sasa uwiano umefikia asilimia 71 ambayo imebaki asilimia moja kufikia viwango vya kimataifa.

Kwa upande mwingine, NHIF imefanikiwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 19.6 kwenye vituo vya afya 94 kwa ajili ya   vifaa tiba au ukarabati wa miundombinu.

Akizungumza kuhusu mwelekeo wa NHIF, amesema wamejipanga kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA, kuanza kutumia akili mnemba pamoja na kuongeza wigo wa wanachama.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi