Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NGOs Zatakiwa Kutunza na Kulinda Maadili ya Kitanzania
Oct 05, 2023
NGOs Zatakiwa Kutunza na Kulinda Maadili ya Kitanzania
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bi. Vickness Mayao wakati alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma kushiriki Kilele cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. (Tarehe 05 Oktoba 2023)
Na Beatrice Lyimo - MAELEZO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwajibika kutunza na kulinda maadili Kwa kuheshimu mila, desturi na tamaduni za kitanzania katika utekelezaji wa afua na miradi mbalimbali.

Dkt. Mpango ameyasema hayo leo OKtoba 5,2023 Jijini Dodoma wakati akifungua Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kusisitiza Mashirika hayo kuzingatia Sheria za nchi na miongozo mbalimbali ambayo inaratibu shughuli za mashirika hayo.

“Mashirika yetu yasiyo ya kiserikali hapa nchini, ninawaomba sana msikubali kutumiwa, tutunze maadili yetu ya kitanzania, tuyalinde, msikubali kuwa tarumbeta za watu wasiotutakia mema; Tanzania ni ya kwetu na watu wasitumie Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupenyeza agenda ambazo haziendani na maadili ya kitanzania”, amesisitiza Dkt. Mpango.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango ameyataka Mashirika hayo kuwajibika na kuwa wazi katika rasilimali zinazopatikana na namna zinavyotumika katika kutekeleza miradi inayokusudiwa.

“Uwajibikaji na uwazi katika Mashirika Yasio ya Kiserikali bado hakuna uwazi wa kutosha, wakati mwingine matumizi ya rasilimali hizo hayawiani na malengo  hivyo ninawasisitiza kuzingatia uwazi kwa kuwa ni sehemu muhimu katika kuwezesha serikali kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu uratibu wa shughuli zinazohusu mashirika hayo”, amefafanua Dkt. Mpango.

Akizungumza kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Mpango amebainisha kuwa, Serikali inaendelea na kuhimiza upandaji wa miti na shughuli za maendeleo katika kukabiliana na athari hiyo, hata hivyo  amezipongeza  NGOs ambazo zinatekeleza afua hizo na kutoa wito kwa mashirika hayo kuendelea kutoa elimu kwa wanachi kuhusu utunzaji wa  mazingira.

Mbali na hayo, Dkt. Mpango ameelekeza Mamlaka za Mikoa na Wilaya kufanya kazi kwa ukaribu na Mashirika hayo.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ameeleza kuwa, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya utendaji kazi, ikiwemo kuanzisha Madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Wizara, Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, pamoja na kuimarisha Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuongeza Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika hayo ambayo ni nyenzo muhimu itakayosaidia kutambua mahali yalipo, pamoja na miradi na afua inayotekelezwa na Mashirika hayo.

“Kwa kuwa Ramani hiyo itatumiwa na wadau kupitia teknolojia rahisi ya kiganjani, itaziwezesha Taasisi za Serikali, Wadau na Jamii kwa ujumla kupata taarifa za Mashirika hayo kwa ajli ya upangaji wa mikakati mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopo, sambamba na kujenga ubia wenye tija na Mashirika hayo”, amebainisha Dkt. Gwajima.


Aidha, Ramani ya Kidijitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, itakayosaidia kutambua mahali yalipo Mashirika pamoja na miradi na afua zinazotekelezwa na Mashirika hayo imezindulia wakati wa funguzi wa jukwaa hilo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi