Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nelson Mandela Yatekeleza Matakwa ya Mikataba Mbalimbali Kuwainua Wanawake
Mar 08, 2024
Nelson Mandela Yatekeleza Matakwa ya Mikataba Mbalimbali Kuwainua Wanawake
Wanawake kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wakiwa katika picha ya pamoja ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2024 jijini Arusha.
Na Lorietha Lawrence

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela inaendelea kutekeleza matakwa ya mikataba mbalimbali ya kimataifa, kitaifa na kikanda pamoja na sera mbalimbali zinazolenga kuwainua wanawake kuleta usawa katika jamii .

Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Maulilio Kipanyula wakati akizungumza na wanawake katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo Machi 8, 2024 jijini Arusha .

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Maulilio Kipanyula akizungumza na wanawake wa taasisi hiyo (hawapo katika picha) wakati wa semina elekezi katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2024 jijini Arusha .

Prof. Kipanyula anaeleza kuwa, ili kauli mbiu ya mwaka huu iweze kutekelezeka ipasavyo, ni dhahiri kwamba inahitajika uwekezaji zaidi kwa wanawake ili kuwaongezea uwezo wa kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kuwahamasisha kutumia teknolojia kwa kuongeza tija katika uzalishaji hivyo kukuza kipato chao.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof, Maulilio Kipanyula akikata keki kuashiria ufunguzi wa semina elekezi katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2024 jijini Arusha.

“Tuchukue hatua leo kuwekeza nguvu zaidi kuhakikisha kuwa wanawake wanapata nafasi wanayostahili katika kuleta mabadiliko na kuchangia maendeleo ya taifa hasa katika nyanja ya sayansi, teknolojia, hisabati, uhandisi na ubunifu ambazo ni nguzo muhimu katika kuwajengea wanawake uwezo kuharakisha maendeleo ya taifa letu na dunia kwa ujumla”, anasema Prof. Kipanyula

Anazidi kufafanua kuwa uongozi wa taasisi unathamini mchango wa wanawake katika kuhakikisha taasisi inazidi kusonga mbele katika eneo la utafiti, na hilo limejidhihirisha wazi kupitia tuzo mbalimbali walizopata wanasayansi wanawake kutoka katika taasisi ambazo zimeweka alama kwa taifa.

Mwendesha Shughuli (MC), Analyse Ichwekeleza akiongea na wanawake wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wakati wa semina elekezi iliyoandaliwa na taasisi kwa kushirikiana na Mradi wa HEET na kituo cha Umahiri CREATES-FNS ikiwa ni kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2024.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu na Utafiti Prof. Revocatus Machunda kwa niaba ya Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango, Fedha na Utawala amewataka wanawake kuwa mabalozi wazuri kuhakikisha mabinti wanapenda masomo ya sayansi ili kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya semina elekezi kwa uratibu wa uongozi wa taasisi, Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Elimu ya Juu (HEET) na Kituo cha Umahiri wa Maendeleo ya Kilimo na Lishe ya Chakula (CREATES-FNS) ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa na watoa mada ikiwemo mwanamke kujipenda, unyanyasaji wa kijinsia, uchumi binafsi na kuhimiza masuala ya Sayansi, Hisabati, Uhandisi na Teknolojia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi