Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limesema kwamba Watanzania 83,500 wamepata ajira katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini kuanzia mwaka 2015-2022.
Akizungumza leo jijini hapa, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ndg. Beng'i Issa amesema ajira hizo zimetokana na kazi zinazofanywa na NEEC ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji.
"Tunashiriki katika majadiliano kuhakikisha katika kila mradi kunakuwa na mpango wa kuwashirikisha Watanzania," ameeleza Ndg. Beng'i.
Pamoja na hilo, amesema kampuni 11,770 zinazomilikiwa na Watanzania zimeshirikishwa na kwamba bidhaa za ujenzi zinazotumika kwenye miradi mbalimbali zinazalishwa na viwanda vilivyopo nchini.
"Takriban asilimia 70 ya nondo zinazotumika kwenye ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na nondo zinazotumika kwenye ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) zinatoka Tanzania," ameeleza Ndg. Beng'i.
Amearifu kwamba ushirikishwaji wa makampuni ya kitanzania umeongeza idadi ya viwanda vya vifaa vya ujenzi ambapo viwanda vya nondo vimeongezeka kutoka vitano hadi 10.
NEEC ilianzishwa mwaka 2005 ili kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004.