Na Mwandishi wetu- MAELEZO
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi afungua mafunzo kwa wawezeshaji ya kuwapitisha Wakuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia rushwa nchini (TAKUKURU), Kamishna Wasaidizi wa Skauti na Maafisa Elimu kwenye mwongozo wa kufundisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na ruhswa nchini.
Ufunguzi huo umefanyika leo jijini Dodoma ukishirikisha makundi matatu ikiwemo TAKUKURU, Chama cha Skauti Tanzania na Wizara ya Elimu.
Mhe. Ndejembi amesema kuwa, ushirikiano baina ya TAKUKURU na Chama cha Skauti kushirikisha vijana wa skauti kuzuia na kupambana na rushwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa awamu ya tatu (NACSAP III) unaosisitiza ushirikishwaji wa wadau katika mapambano dhidi ya rushwa.
Ameeleza kuwa, hatua ya mkakati huo wa kushirikisha vijana wa skauti katika mapambano dhidi ya rushwa ni hatua ya msingi ya kukabiliana na tatizo la rushwa katika jamii ikizingatia wingi wa vijana katika jamii na nguvu waliyonayo hivyo itaongeza idadi ya washiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na uzalendo nchini.
Pia amesema, rushwa inamadhara kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla ikiwemo vijana, hivyo vitendo vya rushwa vimekosesha wananchi haki ya kupata huduma bora za afya, maji safi na salama, barabara nzuri, fursa za masomo na fursa za ajira, pembejeo za kilimo, mikopo ya kuendesha shughuli za kuiongezea kipato.
“Vijana wengi wa skauti ni vijana waliopo masomoni, na sekta ya elimu ni sekta ambayo haijaachwa salama na rushwa, rushwa katika sekta ya hiyo inahusisha rushwa ya fedha, rushwa ya ngono, matumizi mabaya ya mamlaka na nyingine hudhoofisha sana ubora wa elimu hasa pale inapotumika kununua mitihani, kufaulisha walimu na wanafunzi, kuajiri watumishi au hata kuwapangia majukumu na vituo vya kazi” amefafanua Naibu Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU Neema Mwakalyelye anasema kuwa lengo kuu la mkakati huo ni kuelimisha vijana wa skauti ili kuichukia rushwa ana kushiriki kuzuia na kupambana nayo ingali wakiwa vijana wadogo.
Ameongeza kuwa mwongozo huo umebeba mambo yanayohusu mbinu mbalimbali za ufundishaji na nadharia za mada kuhusu rushwa ikiwa na madhumuni ya kuwajenga vijana kimaadili, misingi ya uadilifu, uzalendo na uwajibikaji.
Takribani washiriki 105 watanufaika na mafunzo hayo ambayo yatafanyika kwa muda wa siku tatu kwa makundi yakiwezeshwa kwa ushirikiano wa Chama cha Skauti Nchini, TAMISEMI, Shirika lisilo la Kiserikali la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) pamoja na TAKUKURU.