Na Beatrice Lyimo
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeanzisha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa kwa kutumia teknolojia mpya na ya kisasa ya kielektroniki kwa njia ya satelaiti na Vishikwambi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Dodoma mrasimu ramani mwandamizi na msimamizi wa Sehemu ya mfumo wa Ukusanyaji na Usambazaji wa taarifa za Kijiografia (GIS) Benedict Mgambi amesema kuwa lengo la mfumo huo ni kuboresha ukusanyaji wa taarifa na tafiti mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Mgambi amesema kuwa teknolojia hii mpya imerahisisha kwa kiasi kikubwa ufanyaji kazi ikilinganishwa na taratibu zilizokuwa zikitumika awali.
“Awali tulikuwa tunatumia teknolojia ya duni ambapo mchakato wake ulihusisha watu wengi, gharama kubwa ila kwa sasa hivi kila kitu kinafanyika eneo husika la tafiti na kutumwa moja kwa moja makao makuu” amesema Mgambi
Aidha Mgambi amesema kuwa zoezi hilo limeshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo, TAMISEMI, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,Wizara ya Maliasili na utalii pamoja na TAMISEMI.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Kijiografia (NBS) Martha Macha amesema kuwa mfumo huo umerahisisha utendaji kazi wao kwani unasaidia kutambua mipaka mbalimbali kati ya kitongoji kimoja na kingine.
“Vifaa hivi vinafanya kazi kubwa kwa muda mfupi na pia vinafanya kazi kwa ubora ule unaohitajika kwa kuona vielelezo mbalimbali vitakavyokuwezesha kufanya kazi kwa urahisi” amefafanu Bi. Macha.
Mpaka sasa vijii vitano vya Sasajila, Suli, Fufu, Champumba na Chiboli Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma vimefanyiwa majaribio ya mfumo huo.