Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ametoa rai kwa jamii ya kitanzania kumlinda mtoto dhidi ya matumizi ya intanenti yanayotokana na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo ikitumika visivyo huchangia kuharibu mila na desturi za kitanzania kwa kufuata tamaduni za kigeni zinazokinzana na maadili ya kitanzania
Rai hiyo ameitoa hivi karibuni jijini Dodoma, wakati akigawa vifaa vya TEHAMA katika shule ya Sekondari ya Chinangali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwa Wizara anayoisimamia kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuendelea kuwapatia watoto wa kitanzania nafasi ya kujifunza na kutumia TEHAMA
Waziri Nape amewataka wazazi na walezi kuadhimisha Siku ya mtoto wa Afrika kwa kutafakari, kutathmini na kukumbushana wajibu wa jamii ya kiafrika katika kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto, haki na maendeleo yao ili kulinda mila na desturi za kiafrika kwa vizazi vijavyo na kuwa na kesho bora na jamii inayojali na kurithisha maadili mema kwa vizazi vijavyo
Ameongeza kuwa, Serikali imewekeza kwenye miundombinu ya elimu ikiwa ni sehemu ya kumuandaa mtoto wa Kitanzania kuchukua dhamana ya kuijenga nchi, ikiwa ni pamoja na elimu ya matumizi ya TEHAMA ambayo hayaepukiki katika ulimwengu wa kidijitali.
“Kama ilivyo maisha bila moto haiwezekana lakini ukitumika vibaya unaweza kuleta madhara makubwa hata kupoteza maisha vivyo hivyo TEHAMA ikitumika vibaya inaweza kumuathiri mtoto wa kiafrika kujifunza tamaduni zisizofaa na matendo ya uovu kupitia mtandao hasa intaneti”, amezungumza Waziri huyo
Amesema kuwa,“Wizara ninayoisimamia ina wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na matumizi salama ya mtandao, lakini pia ni wajibu wa wazazi na walezi wakiwemo walimu kuwalinda watoto wetu dhidi ya changamoto zinazotokana na ukuaji wa TEHAMA na kwa kuchungulia nini watoto wanafanya kwenye mtandao na kutoona aibu kuwaeleza ukweli juu ya faida na hasara za ukuaji wa TEHAMA”.