Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nape Akaribisha Canada Kujenga Viwanda vya Simu
May 26, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Lilian Lundo - MAELEZO

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewakaribisha wawekezaji kutoka Canada kuja kuwekeza katika viwanda vya utengenezaji wa simu janja hapa nchini. 

Nape amesema hayo katika kikao cha kubadilishana uzoefu na Katibu  wa Mambo ya Nje wa Canada, Robert Oliphant ambapo walijadili masuala mbalimbali ya habari na teknolojia ya habari, leo Mei 26, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam. 

"Eneo ambalo tulitamani kama serikali kupata wawekezaji,  ni eneo la upatikanaji  wa simu janja (smart phones na tablets), ili  ziwe bei nafuu na watu waweze kumudu kununua," alifafanua Nape. 

Aliendelea kusema kuwa, kutokana na Tanzania kutokuwa na viwanda vya kutengeneza simu janja imesababisha vifaa hivyo kuwa na gharama ya juu, hivyo kupelekea idadi chache ya Watanzania kuweza kumiliki simu hizo. 

Nape amesema kuwa, ni asilimia 27% tu ya Watanzania ndio wanaomiliki simu janja na asilimia inayobaki wanamiliki simu za kawaida, kutokana na gharama ya simu janja kuwa ya juu. 

"Sasa imefika wakati simu janja zizalishwe hapa nchini, ili bei iwe ya chini na kila Mtanzania aweze kupata kifaa hicho, na hata huduma ikiboreshwa ina maana watu wengi watapata hiyo huduma," alifafanua Nape. 

Kwa upande wake, Katibu wa Mambo ya Nje wa Canada, Robert Oliphant amesema kuwa ili Tanzania iweze kuwa na mawasiliano ya uhakika inatakiwa kuweka vipaumbele eneo la nishati, maendeleo pamoja na watu wenye ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi