Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Pinda Ashiriki Kongamano la Kimataifa Kuhusu Miji Austria
Oct 10, 2024
Naibu Waziri Pinda Ashiriki Kongamano la Kimataifa Kuhusu Miji Austria
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe, Geophrey Pinda (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wanaoshiriki Kongamano la Kimataifa la Miji linaloendelea Jijini Vienna nchini Austria.
Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Pinda anashiriki Kongamano la Kimataifa kuhusu Miji linalofanyika Vienna nchini Austria. 

 

Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu ya "Suluhu Bunifu kwa Miji ya Kesho” linafanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Vienna, Austria kuanzia tarehe 9 hadi 11 Oktoba, 2024 na kuhusisha viongozi na wataalamu wanaohusika na masuala ya usimamizi wa ukuaji na uendelezaji miji kutoka nchi mbalimbali. 

 

Kupitia kongamano hilo, Mhe. Pinda aliwaeleza washiriki namna serikali ya Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyofanya jitihada kukuza na kuendeleza miji.

 

Amezitaja baadhi ya jitihada hizo kuwa ni pamoja na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma, matumizi ya mifumo ya kielektroniki kwenye masuala ya ardhi, uanzishwaji kituo cha taifa cha ubunifu na mafunzo cha taarifa za kijiografia pamoja na maboresho mbalimbali ikiwemo ya Sera ya Taifa.

 

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi ameongeza kwa kusema, kwa sasa Tanzania imeanza pia kutumia teknolojia ya kisasa kutambua wazalishaji taka ngumu ambapo amesema teknolojia hiyo imerahisisha namna ya kuwafikia watumiaji na ukusanyaji wa taka ngumu.

 

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda, katika Jiji la Da es salaam, tathmini inaonyesha kuwa teknolojia hiyo imekuwa na ufanisi kwa asilimia 129 (129%) katika kutambua wazalishaji na maeneo yanayozalishwa taka ngumu kwa wingi ikilinganishwa na  mfumo wa kawaida  uliokuwa ukitumika kukusanya taka ngumu.

 

Akigeukia suala la ushirikishwaji wananchi katika masuala ya uendelezaji miji, Mhe, Pinda, amesema Tanzania imebaini michango mikubwa ya wananchi katika upangaji na uendelezaji miji ambapo wananchi hushirikishwa kikamilifu huku akibainisha kuwa, mfumo huo umeonekana kuleta tija katika upangaji na usimamizi wa miji na kutolea mfano katika Jiji la Arusha eneo la Mianzini ambapo makundi mbalimbali ya jamii yalihusishwa na kushirikishwa katika kuandaa mpango wa uendelezaji wa eneo hilo.

 

“Wazee, vijana, wanawake na viongozi wa eneo husika walishirikishwa na sauti yao kusikika huu nao ni ubunifu mzuri unaleta suluhu kwa miji ya kesho”. Amesema Mhe. Pinda.

 

Amelishukuru Shirika la Kimatifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kuandaa kongamanao hilo muhimu lililowakutanisha pamoja viongozi wanaohusika na masuala ya usimamizi wa ukuaji na uendelezaji miji kushirikishana ubunifu na mbinu mpya ya uendelezaji wa miji ya kesho

 

Lengo la mkutano huo ni kujadili na kushirikishana juu ya Suluhu bunifu kwa miji ya kesho pamoja na kutoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu kwa mustakabali endelevu wa miji kwa watu wote duniani.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi