Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Nyongo Apiga Marufuku Vishoka kwenye Soko la Madini Tunduru
Jun 30, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_53682" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wafanyabiashara wa madini (hawapo pichani) kwenye mkutano uliofanyika katika Soko la Madini la Tunduru Mkoani Ruvuma wenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto tarehe 29 Juni, 2020.[/caption]

Na Greyson Mwase, Tunduru

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amepiga marufuku watu wanaofanya biashara nje ya mfumo wa masoko yaliyoanzishwa maarufu kama vishoka na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Naibu Waziri Nyongo ameyasema hayo mapema leo tarehe 29 Juni, 2020 kwenye mkutano wake na wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini Tunduru ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye soko hilo yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye uendeshaji wa soko hilo.

Katika kikao hicho  Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Ruvuma, Isaack Ngerangera, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Getty Massawe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephraim Mushi na  Afisa Utawala wa Tume ya Madini, Saashisha Mafuwe.

[caption id="attachment_53683" align="aligncenter" width="750"] Sehemu ya wafanyabiashara wa madini wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano uliofanyika katika Soko la Madini la Tunduru Mkoani Ruvuma wenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto tarehe 29 Juni, 2020.[/caption]

Alisema kuwa, katika Soko la Madini la Tunduru wapo watu wasio waaminifu wamekuwa wakifanya biashara ya madini nje ya soko la madini lililoanzishwa na kuongeza kuwa Serikali haitawafumbia macho kwa kuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi kutokana na kukwepa kodi mbalimbali zinazotakiwa kulipwa Serikalini.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inakuja na mkakati mpya wa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa madini wanatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa.

Katika hatua nyingine Nyongo alisema kuwa ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wananufaika na shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliamua kufuta kodi nyingi zilizokuwa kero  kwa wachimbaji wa madini pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini.

  [caption id="attachment_53684" align="aligncenter" width="750"] Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Getty Massawe, akitoa taarifa ya maendeleo ya Soko la Madini la Chunya kwenye mkutano huo. Waliokaa kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Ruvuma, Isaack Ngerangera.[/caption] [caption id="attachment_53685" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro akifafanua jambo kwenye mkutano huo.[/caption]

Katika hatua nyingine, Nyongo aliwataka maafisa madini wakazi nchini kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama na Taasisi nyingine za Serikali.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Nyongo alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkaguzi Msaidizi wa Madini, Athumani Masawe ambaye alituhumiwa na wanunuzi wa madini kuhusika na kufanya biashara nje ya soko kinyume na sheria ya madini.

Aidha amekemea vikali tabia ya viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Wilaya ya Tunduru kuingilia shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini ndani ya Soko la Madini la Tunduru.

Katika hatua nyingine alimpongeza Mkuu  wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwenye sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini  Wilaya ya Tunduru kwa kuingilia shughuli za uendeshaji wa Soko la Madini la Tunduru.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alimpongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kufanya ziara kwenye soko hilo na kutatua changamoto zilizojitokeza na kuongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa  Mkoa wa Ruvuma kwenye usimamizi wa Soko la Madini Tunduru ili liwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi