Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amelitaka Baraza la Wafanyakazi la Sekta hiyo kutafuta suluhu ya changamoto za wafanyakazi na kuweka usawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Mwakibete amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi lililowakutanisha kwa ajili ya kujadili masuala ya wafanyakazi na kupitia mpango wa Bajeti kwa kipindi cha mwaka 2022/2023.
“Hakikisheni mnashughulikia malalamiko ya watumishi sehemu mnazozisimamia ili kuweka usawa na utendaji kazi mzuri kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kupewa nafasi za kujiendeleza kielimu”, amesema Mwakibete.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa kwa sasa Sekta inafanya uhakiki na uchambuzi wa madeni ya watumishi hususan wastaafu na kuweka mikakati thabiti ya kulipa madeni hayo.
“Baraza hili linakutana hapa kwa ajili ya kupitia utekelezaji wa mpango na Bajeti ya Sekta ya Uchukuzi kwa mwaka 2020/2021 ikiwa ni pamoja na masuala mbalimbali yanayowahusu watumishi”, amefafanua Migire.
Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Uchukuzi limeshirikisha Wajumbe wa Baraza ambao ni Wakuu wa Idara na Vitengo, wakuu wa taasisi zote zilizoko chini ya Sekta hiyo pamoja na viongozi wa chama cha wafanyakazi.