Na Faraja Mpina, TARIME
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ameendelea kutoa elimu juu ya manufaa ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi katika ziara yake ya kikazi ambapo mpaka sasa amezuru katika Mikoa ya Mtwara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dodoma, Geita, Kagera, Mwanza na Mara pamoja na Wilaya zake na kuhamasisha utekelezaji wa mfumo huo katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya na Manispaa zote nchini
Amesema kuwa katika ziara zake amefurahishwa kuona baadhi ya Halmashauri wanaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka katika makusanyo yao ya ndani huku akizitolea mfano Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na Mwanza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Nyamagana kwa juhudi walizozionesha katika kutekeleza Mfumo huo.
Akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Tarime na Rorya mkoani Mara, Mhandisi Kundo amefanya mazungumzo na kamati za ulinzi na Usalama za Wilaya hizo na kuelezea kwa kina umuhimu wa Mfumo huo kuwa utazisaidia sana halmashauri katika kuwabainisha walipa kodi na kuweza kukadiria makusanyo ya halmashauri kwa kila mwaka wa fedha
Ameongeza kuwa Mfumo huo utasaidia taasisi za Serikali kama vile Jeshi la Polisi, zimamoto na wataalam wa afya kufika kwa urahisi na kuchukua hatua katika maeneo yenye dharura za uhalifu, wahamiaji haramu, majanga ya moto, dharura za ugonjwa au ajali kwa kufuata taarifa za jina la barabara au mtaa na namba ya nyumba ambayo itakuwa imetolewa na mtoa taarifa.
Mhandisi Kundo amezungumzia mfumo huo kuwa unakwenda kurahisisha kufanyika kwa biashara mtandao kwa sababu una taarifa za kila eneo kama vile barabara, mitaa namba za majengo na makazi ya watu hivyo kurahisisha mfanyabiashara kumfiki8a mteja wake mahali alipo kwa kufuata vibao vinavyoonesha majina ya barabara, mtaa na namba ya nyumba au jengo husika
Aidha, Mhandisi Kundo amesema kuwa taarifa zote zinakuwa zimehifadhiwa katika kanzidata ambapo mtu yeyote akitaka kuzitumia atazipata kupitia Programu Tumizi ya ya simu za mkononi ya NAPA ambayo itampatia mhusika ramani ya kufika pale anapotaka kufika kwa kuingiza taarifa za mtaa au barabara na namba za nyumba au jengo husika
Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo kukamilika kwake kutachochea kukua kwa uchumi wa dijitali kupitia biashara mtandao lakini pia ni Mfumo muhimu sana kwa usalama wa nchi yetu.