Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Mgalu Azindua REA III Mafia
Jul 07, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Veronica Simba – Mafia

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu amezindua rasmi uwekaji wa miundombinu ya umeme wilayani Mafia kupitia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III).

Amefanya uzinduzi huo jana, Julai 6, 2018 katika eneo la Kigamboni, Kata ya Mafia ambapo pia alizungumza na wananchi wake pamoja na wa Kijiji cha Chole.

Naibu Waziri aliwaeleza wananchi kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Nishati, imejipanga kuhakikisha kuwa Vijiji na Vitongoji vyote vinakuwa na umeme ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni, 2021.

“Nia ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali anayoiongoza, ni kuviwashia umeme vijiji na vitongoji vyote nchini, kabla ya Julai 2021.”

Aidha, aliwaeleza wananchi kuwa, Serikali inatambua umeme uliopo sasa katika Kisiwa cha Mafia, hautoshelezi mahitaji hivyo imejipanga kupeleka miundombinu ya umeme wa jua, ambapo kutafanyika uzinduzi wake rasmi mwezi Septemba, mwaka huu.

“Tutaweka Mtambo wa umeme wa jua wenye uwezo wa kuzalisha megawati Tano za umeme. Kabla ya kuanza Mradi huo, tumejipanga kusambaza Paneli za umeme jua katika Taasisi zote za Umma, hususan zilizoko visiwani,” alifafanua.

Kufuatia taarifa ya utendaji kazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wilayani humo, iliyowasilishwa kwa Naibu Waziri na Meneja wa eneo husika, Patience Ndunguru, ambayo ilieleza kuwa moja ya changamoto kubwa za utekelezaji miradi ya umeme kwa wananchi wa Mafia, ni kutokana na wengi wao kutoruhusu mradi kupita katika maeneo yao hadi walipwe fidia; Naibu Waziri aliwataka kuachana mara moja na tabia hiyo kwani inachelewesha maendeleo yao.

“Tunapochelewesha miradi ya namna hii, tunajicheleweshea maendeleo yetu wenyewe.”

Akifafanua kwa wananchi, sababu za Mradi wa REA III kutokuwa na fidia, Naibu Waziri aliwaeleza wananchi kuwa, ni kutokana na gharama zote za Mradi kulipwa na Serikali na kila mwananchi anayetaka kuunganishiwa umeme kutakiwa kuchangia kodi kidogo tu ya shilingi 27,000.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri pia, alichangia Seti mbili za Vifaa vya Taa zinazotumia umeme wa jua kwa kila Zahanati za Vijiji alivyotembelea ambazo ni Chole na Zahanati ya Bwejuu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaib Nnunduma, alimshukuru Naibu Waziri na Serikali kwa ujumla kwa mikakati na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi hususan miradi ya umeme.

Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau, pamoja na kupongeza jitihada za Serikali katika kuwapelekea wananchi wa Mafia nishati ya umeme, aliungana na Naibu Waziri kuwataka wananchi kuachana na utamaduni wa kudai fidia kwa miradi ya maendeleo, hususan Mradi wa Umeme Vijijini.

Naibu Waziri anaendelea na ziara yake wilayani Mafia, ambapo katika siku ya pili, atatembelea maeneo ya Marimbani, Juani na Mlongo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi