Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Katimba Asisitiza Watumishi TSC Kuendelea Kufanya Kazi kwa Bidii
Apr 09, 2024
Naibu Waziri Katimba Asisitiza Watumishi TSC Kuendelea Kufanya Kazi kwa Bidii
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Zainabu Katimba akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), tarehe 08 Aprili, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kiwete jijini Dodoma.
Na Mwandishi wetu – Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Zainabu Katimba amewataka watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo katika Sekta ya Elimu.

Naibu Waziri Zainabu ametoa kauli hiyo tarehe 08 Aprili, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kiwete jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa TSC ndiyo yenye dhamana ya kusimamia walimu ambao wanachukua zaidi ya nusu ya watumishi wa umma nchini, hivyo ni vema kufanya kazi kwa bidii ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa amani na utulivu.

“Natumia nafasi hii kumpongeza kwa dhati Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutimiza miaka mitatu tangu alipoanza kuliongoza Taifa la Tanzania. Katika kipindi cha uongozi wake tumeshuhudia akitoa kipaumbele kikubwa katika sekta ya elimu, watumishi wa umma wamepandishwa vyeo kwa mfululizo,” amesema.

Mhe. Zainabu amesema katika kudhihirisha hilo, walimu 227,383 wamepandishwa vyeo na walimu 37,879 waliajiriwa katika uongozi wa Rais Samia.

“Ukiangalia juhudi hizo za Rais wetu, ni muhimu kwenu ninyi watumishi kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kikamilifu na kusaidia kutatua changamoto zinazorudisha nyuma utendaji kazi wa walimu,” ameongeza.

Aidha, Naibu Waziri ameipongeza TSC kwa kujenga mfumo wa kielektoniki wa Teachers’ Service Commission Management Information System (TSCMIS), kusimika mtandao wa intaneti kwenye baadhi ya ofisi za wilaya pamoja na kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la TSC makao makuu ambalo limefikia asilimia 37.

“Ninawapongeza kwa kuendelea kutekeleza majukumu yenu hususan katika masuala ya matumizi ya teknolojia ambayo yanarahisisha utekelezaji wa majukumu yenu. Kuhusu mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi unaoendelea, ninamtaka Mkandarasi, SUMA JKT kuongeza kazi ya ujenzi ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika katika muda ulioainishwa kwenye mkataba,” amesema.  

Akizungumzia kuhusu Baraza la Wafanyakazi, Mhe. Zainabu ameipongeza TSC kwa kuwa na Baraza la Wafanyakazi ambalo lipo hai huku akiwataka wajumbe wa Baraza hilo kutumia mkutano huo kuwasilisha vyema hoja za watumishi wengine ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

Akimkaribisha Naibu Waziri huyo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde amesema Rais Samia ameonesha juhudi kubwa katika kushughulikia changamoto za walimu zikiwemo kupandishwa madaraja, kubadilishiwa cheo (recategorization), kulipa madai ya uhamisho, malipo ya fedha za likizo pamoja na malimbikizo ya mshahara.

 

“Hivi karibuni tulikuwa na zoezi kubwa la kubaini walimu wenye changamoto katika madaraja yao ambapo Maafisa Utumishi wa Mikoa na Halmashauri walihakiki taarifa za walimu wote nchini, na uhakiki huo imewasilishwa Ofisi ya Rais – UTUMISHI kwa hatua zaidi,” amesema Dkt. Msonde.

 

Awali, Katibu TSC, Mwl. Paulina Nkwama alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada nyingi katika kuimarisha elimu na walimu nchini ikiwemo kulipa malimbikizo ya madai mbalimbali ya mishahara na yasiyo ya mishahara.

 

Amesema jitihada hizo ni pamoja na kuajiri walimu 14,949 katika mwaka wa fedha wa 2020/21; 9,800 mwaka wa fedha wa 2021/22 na walimu 13,130 kwa mwaka 2022/23 ili kukabiliana na upungufu wa walimu.

 

Ameongeza kuwa serikali pia imeweka punguzo la kodi katika mishahara ya watumishi kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8 na kuondoa tozo ya thamani ya elimu ya juu pamoja na wategemezi wa bima kutoka umri wa miaka 18 hadi 21.

 

Mwl. Nkwama amesema mafanikio mengine ya Tume katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita ni pamoja na watumishi wa Tume 305 kupandishwa vyeo pamoja na kupatiwa vitendea kazi zikiwemo kompyuta mpakato 159, vishikwambi 550, pikipiki 137, basi dogo moja (1) na magari mawili (2).

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi