Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Katambi Abainisha Utekeleaji wa Maagizo ya Mkutano wa Wenye Ulemavu Ikulu
Jun 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Patrobas Katambi amebainisha utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati alipokutana na wenye Ulemavu mnamo mwezi Machi, mwaka huu, Ikulu Chamwino Dodoma.

Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kupokea changamoto zinazowakabili wenye ulemavu nchini na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi.

Akiongea wakati wa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Wafanyakazi wenye Ulemavu tarehe 27 Juni, 2022 jijini Dodoma, Mhe. Katambi amebainisha kuwa Mhe. Rais Samia ametoa zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kukarabati vyuo vya Ufundi Stadi kwa wenye Ulemavu ambapo ukarabati huo unaendelea katika Mkoa wa Tabora, Singida, Dar es salaam na Mtwara.

Aidha, amefafanua kuwa vitajengwa vyuo vipya mkoani Kigoma na Mwanza huku chuo cha Masiwani Tanga tayari kimeshafunguliwa.

Mhe. Katambi ameomgeza kuwa tayari Serikali imeiwezesha Hospitali ya KCMC ili iweze kuzalisha mafuta yanayosaidia kukinga mionzi ya jua kwa wenye ulemavu wa ngozi, lengo likiwa ni uhamasishaji wa uzalishaji wa ndani wa mafuta hayo ili kuleta unafuu na uhakika wa upatikanji wake. 

Aidha, Mhe. Katambi ameeleza kuwa katika kuhakikisha haki inatendeka kwa Wenye Ulemavu, tayari Mhe. Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya kupitia Sera na Sheria zinazo wahusu Wenye Ulemavu, ikwemo; Waraka wa utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010, Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. 

Sera ya Huduma kwa Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu pamoja na Sera ya Taifa ya Vijana zinaendelea kufanyiwa mapitio.

Aidha, katika hatua nyingine Mhe. Katambi amesisitiza ujenzi wa majengo ya Serikali kuhakikisha unazingatia miundombinu rafiki kwa wenye ulemavu. Hivyo amezitaka Mamlaka za Serikali na zisisizo za serikali kuhakikisha zinatekeleza Sera na Sheria za wenye Ulemavu nchini.

“Sera na Sheria yetu inasema 3% katika utoaji wa ajira kwa wenye ulemavu, tunaenda kufanya ukaguzi kwa  kuanza na mamlaka za serikali kuona ni namna gani zinatekeleza  pia tutaenda kukagua Sekta Binafsi. Tunazitaka Mamlaka, Asasi na Taasisi zisizo za serikali kutekeleza sheria za Wenye Ulemavu kama anavyotaka Mhe. Rais Samia”

Mhe. Katambi ametaja hatua nyingine ambazo serikali inaendelea kutekeleza ni katika sekta ya elimu pamoja na Bima. Pia, suala la vifaa vya watu wenye Ulemavu jinsi ya kuangalia namna bora ya kuhakikisha vinapatikana kama serikali inavyotaka.

Katika hatua nyingine, Mkurungenzi wa Taasisi ya Ikupa Trust Fund ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Stella Ikupa, ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassann kwa kuyapa kipaumbele masuala yanayowahusu wenye Ulemavu nchini. Aidha, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuajiri wenye Ulemavu.

Mkutano huo ulioandaliwa na kuratibiwa na Taasisi ya  Ikupa Trust Fund, Kaulimbiu yake ni; “Stahiki Bora, Haki ya kuajiliwa, na Mazingira rafiki ya kazi  kwa Watu Wenye Uleamavu”

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi