Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Katibu Mkuu Yakubu: Tanzania Ipo Mstari wa Mbele Kueneza Lugha ya Kiswahili
Mar 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eleuteri Mangi, WUSM-Arusha

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu amesema Serikali ya Tanzania ipo mstari wa mbele kushirikiana na Redio China Kimataifa ili kuendelea kukuza lugha adhimu ya Kiswahili duniani.

Naibu Katibu Mkuu, Bw. Yakubu amesema hayo alipokutana na kufanya kikao Machi 16, 2022 na Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa, Ofisi ya Nairobi, Bi. Du Shunfang ambaye ni miongoni mwa washiriki wa Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani linaloendelea katika Kituo cha Mikitano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha kwa siku tano kuanzia Machi 14-18, 2022.

“Tumeona tutumie fursa hii ya uwepo wako hapa nchini kwenye Kongamano hili ili tuone namna bora na maeneo ya ushirikiano katika kukuza na kuendeleza lugha aushi ya Kiswahili duniani kupitia Redio China Kimataifa”, amesema Naibu Katibu Mkuu, Bw. Yakubu.

Katika mazungumzo yao, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Yakubu na Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa, Bi. Du Shunfang wamekubaliana kuwa wataona namna bora ambayo Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) watatoa maudhi ya vipindi vya kukuza na kuendeleza Kiswahili nchini China na Redio China Kimataifa watatangaza na kusambaza maudhui hayo.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Yakubu ameongeza kuwa kuna haja ya kuwa na Kongamano la Kiswahili ambalo litafanyika mara moja kwa mwaka nchini China ili kuendelea kuongeza wigo wa kukuza lugha ya Kiswahili nchini humo na kutoa fursa ya watu wengi kushiriki na kujifunza istilahi, misemo, methali, nahau na maneno mengine ambayo yatatumika kulingana na muktadha na mazingira ya nchi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa, Ofisi ya Nairobi, Bi. Du Shunfang amesema kuwa Kiswahili kina soko kubwa nchini China katika maeneo mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara, kufundisha katika shule na vyuo mbalimbali vinavyofundisha lugha ya Kiswahili kama somo na lugha ya kigeni kwa ajili ya biashara.

Katika kueneza Kiswahili nchini China, yeye ametafsiri vitabu sita vya Kiswahili kwenda lugha ya Kichina na Kichina kwenda Kiswahili na kuna watu wanafanya utafiti na kuandika vitabu vya Kiswahili na chanzo cha lugha ya Kiswahili ni Utamaduni.

“Mahitaji ya kufundisha lugha ya Kiswahili bado ni makubwa, kwa sasa lugha ya Kiswahili inafundishwa kupitia mashirika ya kimataifa na kuna taasisi tatu China zinafanya utafiti katika mambo ya Afrika ikiwemo Kiswahili”, amesema Bi. Du Shunfang.

Bi. Du Shunfang amesema kuwa Redio China Kimataifa inawasikilizaji wengi kupitia mtandao wa facebook zaidi ya milioni mbili na kuongeza kuwa Wachina wote wanaokuja Afrika wanapenda kujifunza lugha ya Kiswahili na kuna wataalamu zaidi ya 200 huku lugha hiyo ikianza kufundishwa nchini humo tangu miaka ya 1960.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa, Bi. Consolata Mushi amesema Baraza hilo litaandaa vipindi maalumu vya kufundisha Kiswahili kwa wageni ambavyo vitarushwa kupitia Redio China Kimataifa.

Zaidi ya hayo, Bi. Consolata amesema kuwa Baraza katika vipindi vyake watakavyoviandaa watatumia maneno rahisi ambayo yatasaidia watu wengi kujifunza lugha ya Kiswahili na hivyo lengo la kueneza lugha hiyo kimataifa kufikiwa na kuenea duniani ikizingatiwa chombo cha habari pamoja na mitandao ya kijamii ndiyo njia rahisi ya kuwafikia watu wengi kwa mara moja.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi