[caption id="attachment_1652" align="alignnone" width="750"] Rais Mstaafu wa awamu ya pili Dkt. Ali Hassan Mwinyi akiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na Mbunge wa Kigamboni Kitwana Kondo katika makaburi ya Tambaza yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.[/caption]
Na. Eliphace Marwa
RAIS Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ameongoza mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam katika maziko ya mwanasiasa mkongwe na aliwayewahi kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, marehemu Kitwana Kondo aliyefariki dunia jana.
Mbali na Mwinyi wengine waliohudhuria maziko hayo yaliyofanyika katika makaburi ya Tambaza ni Makamu wa Rais Mstaafu, Mohammed Gharib Bilal, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Salim Ahmed Salim na Edward Lowassa, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na wengine.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Mzee Mwinyi alisema, marehemu Kondo alikuwa ni mtu ambaye alijitoa katika kulitumikia taifa kwa moyo wake, hivyo mchango wake ni mkubwa katika kulitumikia taifa na hasa wakazi wa jiji la Dar Es Salaam.
"Alikuwa ni rafiki yangu ambaye tumefahamiana kwa muda mrefu, tumepoteza mtu muhimu sana, lakini kazi ya Mungu haina makosa, tumuombee kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi," alisema Mzee Mwinyi
[caption id="attachment_1654" align="alignnone" width="750"] Mwili wa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na Mbunge wa Kigamboni Kitwana Kondo ukiwa umeingizwa kwenye kaburi tayari kwa ajili ya maziko katika makaburi ya Tambaza yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.[/caption]Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana alisema, taifa na hasa wakazi wa Dar es Salaan wamepata pigo kubwa kwa kumpoteza mzee huyo ambaye bado busara zake zilikuwa zikihitajika.
"Alikuwa ni kiongozi wa jamii, alikuwa ni mwalimu wa watu wengi katika mambo mbalimbali, ni msiba mkubwa lakini nj kazi ya Mungu, tuendelee kumuombea apumzike kwa amani," alisema Kinana.
Naye, Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa alisema, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mzee Kondo ni vema uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuangalia namna ambavyo barabara moja ya jiji hilo ikapewa jina la KK ikiwa ni kuheshimu na kutambua mchango wake.
[caption id="attachment_1653" align="aligncenter" width="750"] Jeneza lilobeba mwili wa Marehemu Kitwana Kondo likiwa limebebwa kuelekea katika msikiti wa Tambaza uliopo upanga jjini Dar es Salaam tayari kwa kufanyiwa ibada.Picha Emmauel Massaka,Globu ya jamii[/caption]Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema, mchango wa Mzee katika taifa ni mkubwa ikiwemo kuleta na kudumisha uhuru wan chi hii.
Akieleza chanzo cha kifo cha baba yake, mtoto wa kwanza wa marehemu, Stara Kondo alisema baba yake aliumwa kwa muda mrefu na madaktari walisema alipata kiharusi na shinikizo la damu.
Mzee Kitwana Kondo aliumwa kwa muda mrefu na Mei 18 mwaka huu alipelekwa hospitali ya Hindul Mandal na kulazwa na juzi alifariki dunia.