Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mzabuni na Watumishi Wanne Igunga Waswekwa Mahabusu kwa Tuhuma za Udanganyifu
Sep 20, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent – RS, TABORA.

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na Mzabuni Muhoro Traders kwa tuhuma za udanganyifu wa ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 23.2.

Agizo hilo limetolewa leo mjini Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Amesema kuwa kwa nyakati tofauti za kuanzia Januari  na Machi mwaka huu watumishi walikula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu jumla ya shilingi 23,202.500.00 mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.

Mwanri anaongeza kuwa watumishi hao waliagiza vifaa hivyo kutoka kwa Mzabuni Muhoro Traders wa Igunga lakini havikuwahi kupokelewa na Halmashauri ya Igunga lakini kwenye vitabu vya Afisa Ugavi na yule wa Bohari walikiri kupokea katika vitabu vyao.

“Naagiza watumishi hao wanne wasimamishwe kazi na wakamatwe wao na Mzabuni Muhoro Traders kisha wawekwe ndani kwa ajili ya kufikishwa Mahakamani ili wajibu tuhuma zinazowakabili” anasema Mkuu huyo wa Mkoa.

Anasema kuwa katika hati namba ya malipo namba 2071-1457 watuhumiwa walichukua shilingi 9,250,000/-, hati namba 2017-1457 walijipatia shilingi 6,850,000/- na hati ya malipo namba 2017-1453 shilingi 7,102,500/- na kusababishia Halmashauri hasara hiyo.

Mwanri amewataja waliokamatwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga Godfrey Mgongo, Afisa Ugavi Mohamed Mtao aliyekuwa Mhasibu wa Idara ya Afya sasa yuko TARURA Richard Byelembo na Boharia wa Idara ya Afya Jones Lotto.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza pia Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga wa sasa Dkt. Bonaventura Kalumbete ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri amewaagiza kushughulikia tatizo la ukosefu wa dawa katika Zahanati kwa sababu tayari Halmashauri hiyo imepokea milioni 550 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi