[caption id="attachment_35236" align="aligncenter" width="750"] Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Tume zilizopo jijini Dodoma[/caption]
Na Greyson Mwase, Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula leo tarehe 13 Septemba, 2018 amekutana na Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya jijini Dodoma. Lengo la ziara ya Balozi Arya kwenye Ofisi ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini lilikuwa ni kujitambulisha pamoja na kufahamu majukumu ya Tume.
Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Kikula alieleza kuwa Tume ya Madini imejipanga kusimamia Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 na kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya madini nchini
Alisema Sheria ya Madini ina matakwa yake kama vile local content, utoaji wa huduma kwa jamii kwenye shughuli za uchimbaji madini (corporate social responsibility) na kiapo cha uadilifu kwenye shughuli za uchimbaji madini (integrity pledge)
[caption id="attachment_35234" align="aligncenter" width="750"] Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akielezea majukumu ya Tume ya Madini kwa Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (hayupo pichani)[/caption]Alisema kuwa Tume imejipanga pia kutoa leseni haraka iwezekanavyo na kuwasaidia wachimbaji wadogo.
Akizungumzia namna Tume ya Madini ilivyojipanga katika kutatua changamoto ya migogoro kwenye Sekta ya Madini Nchini, Profesa Kikula alisema kuwa Tume inaandaa mpango wa kutatua migogoro kuanzia katika ngazi ya kijiji, kata, wilaya na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa migogoro mingi inatatulika katika mamlaka za Vijiji, Kata na Wilaya
Aidha, Profesa Kikula alimwomba Balozi wa India kuendelea kutoa ufadhili kwa wataalam wa Tume ya Madini hususan katika maeneo ya Uchimbaji wa Madini kwa kutumia teknolojia ya kisasa, Usimamizi wa Rasilimali Watu na maeneo mengine ili kukuza Sekta ya Madini Nchini.
“ Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, na kama Tume kwa kushirikiana na Wizara ya Madini tumejipanga kuhakikisha tunakuwa na wataalam wenye weledi kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini. Hivyo basi mafunzo kwa wataalam tunayapa kipaumbele sana,” alisisitiza Profesa Kikula.
[caption id="attachment_35235" align="aligncenter" width="750"] Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula zilizopo jijini Dodoma[/caption]Katika hatua nyingine, Profesa Kikula alimwomba Balozi wa India kuendelea kutangaza Sekta ya Madini Nchini na kusisitiza kuwa Tanzania ina maeneo mengi yenye madini yaliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)
Alisisitiza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali.
Wakati huo huo Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya alisema kuwa nchi ya India ipo tayari kushirikiana na Tume ya Madini hususan katika Sekta ya Madini na kusisitiza kuwa wapo tayari kutoa ufadhili kwa watumishi wa Tume.
Aliendelea kusema kuwa nchi ya India imekuwa ikitoa mafunzo ya muda mrefu hususan katika ngazi za Shahada za Uzamili na za Uzamivu katika vyuo bora na kusisitiza kuwa itaendelea na mpango wake wa kutoa mafunzo hususan kwenye masuala ya madini.
Katika hatua nyingine, Balozi Arya alimpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kwa kuteuliwa kuongoza Tume hiyo pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Tume ya Madini kwenye uboreshaji wa Sekta ya Madini Nchini.