Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mwenge wa Uhuru Kutembelea Miradi ya Bilioni 10 Mkoani Rukwa
Sep 21, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Mwenge wa Uhuru Kitaifa unategemewa kutembelea miradi 18 ya maendeleo na vikundi saba vya wajasiriamali mkoani Rukwa kwa pamoja vikiwa na thamani ya shilingi bilioni 10.55.

Miradi hiyo itawekewa mawe ya msingi, itakaguliwa na kuzinduliwa katika Wilaya tatu za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti  alieleza hayo Septemba 20, 2021  baada ya kukabidhiwa mwenge  huo  na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba katika sherehe ya  makabidhiano katika kijiji cha Tunko kilichopo katika  Wilaya ya Sumbawanga mpakani na Mkoa wa Songwe.

Akizungumzia mchanganuo wa uchangiaji wa miradi hiyo alisema wananchi wamechangia shilingi 101,496,100.00, Halmashauri zimechangia shilingi 183,094,374/-, Serikali Kuu umechangia shilingi 9,986,485,860/- huku wadau wa maendeleo na wahisani wamechangia Sh 286,174,244.07

"Mwenge wa Uhuru Kitaifa utakimbizwa kilomita 544.9 katika wilaya tatu za kiutawala" alieleza.

Alisema mkoa umejipanga kikamilifu katika kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2021 " TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu, Itumike kwa usahihi na uwajibikaji".

Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa alisema katika kipindi cha Juni 2020 hadi Julai 2021 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TaKUKURU) mkoa uliokoa kiasi cha shilingi 502,952,380 ambazo shilingi 334,464,330 zilidhibitiwa na shilingi 168,488,000 zilikuwa fedha taslimu.

Kwa upande wake Kiongozi wa Taifa wa Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Luteni Josephine Mwambashi alizitaka halmashauri kuhakikisha nyaraka zote muhimu zinakuwepo katika miradi itakayokaguliwa.

Pia alizitaka halmashauri katika miradi yote itakayokaguliwa na mwenge huo wawepo wataalamu ambapo watatoa taarifa za kina pia wawe na uwezo wa kujibu maswali watakayoulizwa na wakimbizi Mwenge Kitaifa.

Ukiwa katika halmashauri ya  Wilaya ya Sumbawanga  Mwenge wa Uhuru umezinduka jengo la ofisi ya Mthibiti Ubora wa Elimu katika mji mdogo wa Laela ambalo ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi milioni 169.2.

Pia utazindua vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu katika Shule ya Sekondari Sumbawanga ambao ujenzi wake umegharibu shilingi milioni 44 na utakagua barabara ya Mpanda 'Road' - Katandala Mission - Mashine za Mpunga- Majengo ambao ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 7.9.

Mwenge wa Uhuru ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1961 mbio zake zilianza rasmi mwaka 1964 huu ukiwa ni mwaka 29 tangu mbio za Mwenge wa Uhuru zirejeshwe chini ya uratibu na usimamizi wa Serikali

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi