Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mwanri: Bodi ya Pamba Waongezeeni Wakulima Mbegu za Pamba
Nov 29, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_23791" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akihamasisha ulimaji wa zao la Pamba kwa wakulima wa Wilaya ya Urambo Mkoani humo wakati wa ziara yake ya kikazi kuhamishisha shughuli za maendeleo.[/caption]

Na: Tiganya Vincent; RS-TABORA

BODI  ya Pamba Tanzania imetakiwa kuongeza mbegu za pamba kufuatia wakazi wengi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Tabora kujitokeza kwa wingi kutaka kulima zao hilo katika msimu wa kilimo ulianza hivi karibuni.

Kauli hiyo ilitolewa jana Novemba 28, 2017 na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa mkutano wake na wanavijiji wa Wilaya ya Urambo waliojitokeza na kumweleza kero mbalimbali ikiwemo uhaba wa kuwa mbegu za pamba kufuatia wengi wao kuonesha nia ya kulima zao hilo.

Alisema kuwa baada wakulima wengi kupatiwa elimu ya uhamasishaji juu ya kilimo cha kisasa cha zao hilo ikiwemo uzingatiaji wa sheria na kanuni za ulimaji wa pamba kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wanakijiji kutaka kulima zao hilo.

[caption id="attachment_23792" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa mkoa huo Aggrey Mwanri alipofanya ziara katika wilaya hiyo kuhamasisha shughuli za maendeleo ikiwe kilimo cha zao la Pamba. (Picha na: RS- Tabora)[/caption]

Mwanri alisema kuwa si vema kuwakatisha tamaa wakulima hao kwa sababu ya ukosefu wa mbegu na dawa za kuua wadudu, hivyo  ni vema Bodi ikalishughulikia suala hilo kwa haraka zaidi.

“Bodi nawaombeni sana msije mkanifanya nionekane mwongo kwa kuwaambia wakulima kuwa mbegu zitapatikana na kisha zisifike …hawataniamini tena” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema kuwa Mkoa wa Tabora ndio uliochaguliwa kuwa mzalishaji wa mbegu za pamba na kitalu cha taifa  kwa ajili ya maeneo mengine nchini, hivyo mbegu pekee inayohitajika kupandwa ni UKM08 katika maeneo yote.

Mwanri alitoa wito kwa Bodi hiyo kuhakikisha kuwa upungufu wa mbegu hizo unaondolewa na zinawafikia wakulima mapema kwa sababu mvua zimeshaanza kunyesha na kuna baadhi ya maeneo mkoani humo zinakuwa ngumu kupitika katika kipindi hicho.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina Kwingwa alisema kuwa katika msimu ujao wa kilimo makisio yao ilikuwa kupokea tani 31,020 lakini hadi sasa wamepokea tani 19,398 na  kusambazwa katika vijiji 56 kati ya 57 vilivyokisiwa kulima zao hilo.

Alisema kulingana na hamasa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa katika maeneo mbalimbali wakulima wengi wamehamasika ambapo wameongezeka kutoka 4,268 hadi kufikia 4,689.

Kwingwa alisema kuwa hali hiyo inawafanya wanahitaji nyongeza ya tani 36 za mbegu ili waweze kukamilisha kwa wakulima wote.

Naye Meneja wa Bodi ya Pamba Tanzania, Kanda ya Magharibi Jones Bwahama alisema kuwa hakuna mkulima ambaye hatashindwa kulima zao hilo kwa sababu ya kukosa mbegu za pamba.

Alisema kuwa nyongeza ya mbegu za pamba zimeshaanza kupelekwa katika maeneo ambayo makisio yameongezeka na zitawafikia wakulima wakati wowote kuanzia sasa.

Bwahama aliongeza kuwa wakati wakiendelea kusambaza mbegu katika maeneo ambayo yanakabiliwa na upungufu, Kampuni ya Usambazaji Mbegu ya Quoton Tanzania Limited  iliyopewa jukumu la kuandaa mbegu za pamba mkoani humo inaendelea na zoezi la kuandaa mbegu zaidi ili kukabiliana na upungufu utakaojitokeza.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Adam Malunkwi alitoa rai kwa wakulima kuzingatia maelekezo ya Mkuu wa Mkoa ili waweze kulima na kuzalisha mazao bora.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi