Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atakumbukwa kwa namna alivyojitoa muhanga kupigania ukombozi na ujenzi wa Taifa hili.
Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo katika sherehe ya kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Mawalimu Julius Kambarage Nyerere, hafla iliyofanyika Msasani nyumbani kwa Hayati Mwalimu Nyerere.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa Hayati Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ndio waliosimamisha nguzo imara za Muungano ambapo wiki hii inasherehekewa miaka 58 tangu kuasisiwa kwake.
Rais Dkt. Mwinyi ambaye amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi alisema kuwa katika kipindi chote cha uhai wake Mwalimu Nyerere alifanya kila linalowezekana kwa ajili ya kuwaunganisha Watanzania akiamini kwamba umoja, upendo na mshikamano pamoja na kudumisha amani ni msingi muhimu kwa maendeleo ya Taifa hili huku akieleza jinsi alivyochukia uonevu, dhulma na ubaguzi wa aina zote.
Aliongeza kuwa Mwalimu alichagua lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa akiamini kwamba ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha Watanzania pamoja na utamaduni wao.
Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa Hayati Baba wa Taifa alikuwa ni Mwanafalsafa wa masuala mbali mbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambaye alitumia uhai wake kusisitiza umuhimu wa kuwa na siasa na mipango ya kujenga uchumi unaojitegemea pamoja na matumizi ya rasilimali zilizopo nchini.
Alisema kuwa Hayati Mwalimu Nyerere aliamini umuhimu wa kuimarisha misingi ya utawala bora kwa kupiga vita vitendo vya rushwa, uzembe, ufisadi, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma.
“Tumkumbuke Hayati Mwalimu Nyerere kwa juhudi zake za kuongoza mapambano ya kupigania uhuru barani Afrika na kuimarisha umoja wa Waafrika (OAU)”, alisema Rais Dkt. Mwinyi.
Aidha, alisema kuwa kwa upande wa jamii, Marehemu Mwalimu atakumbukwa kwa tabia njema, upole na ucheshi aliokuwa nao kwnai alikuwa ni mwalimu na mlezi mzuri ambapo pia, hekima na busara zake katika uongozi ndizo zilizoleta amani, umoja na mshikamano hapa nchini.
Rais Dkt. Mwinyi alitoa shukurani kwa Mama Maria Nyerere na Wanafamilia kwa kuandaa shughuli hiyo ya kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Marehemu Mwalimu Nyerere.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alipokea salamu za upendo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika tukio hilo lililowakutanisha wanafamilia, marafiki wa marehemu, viongozi aliofanya kazi nao pamoja na wananchi mbalimbali.
Nae Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa alieleza kwamba kuna kila sababu za kumkumbuka Hayati Mwalimu Nyerere hasa ikizingatiwa alikuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Bara la Afrika hasa katika nchi za Kusini mwa bara hilo.
Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba nae kwa upande wake alieleza historia historia ya Mwalimu Nyerere katika uhai wake na jinsi alivyopinga ubinafsi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama kwa upande wake alieleza jinsi Hayati Mwalimu Nyerere alivyopinga maradhi, ujinga na umasikini huku akiahidi kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kumtunza Mama Maria Nyerere.
Rais Dkt. Mwinyi mara baada ya kufika nyumbani hapo alitembelea banda maalum lililowekwa kumbukumbu mbalimbali za Hayati Mwalimu Nyerere na kupata maelezo kutoka kwa Sophia Fredy wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Mapema akitoa ukaribisho pamoja na neno la shukurani mtoto wa Hayati Mwalimu Nyerere, Makongoro Nyerere alisema kuwa sherehe hizo ni wazo la Mama Maria Nyerere la kumkumbuka mumewe Hayati Mwalimu Nyerere kwa kutimiza miaka 100 tokea kuzaliwa kwake.
Katika sherehe hizo, Mama Maria Nyerere alitoa zawadi za mbuzi watato kwa viongozi mbali mbali ambapo Rais Dkt. Mwinyi alipewa mbuzi dume.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,
Ikulu Zanzibar.