Na. Geofrey A. Kazaula
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi ambaye ni Mbuya’s Contractors Company Limited anayejenga Barabara za Mjini-Matai katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kukamilisha mradi unaotokana na ahadi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda kulingana na mkataba.
Mtendaji Mkuu amemuelekeza Mkandarasi huyo kuhakikisha anazingatia viwango katika kutekeleza mkataba huo ili barabara ziweze kuwa na ubora unaotakiwa.
‘‘Unatakiwa kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati lakini pia unazingatia viwango vinavyotakiwa, na mimi mwenyewe nitarudi hapa kujiridhisha’’ alisema Kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Seff alitembelea miradi ya barabara na madaraja katika Halmashauri mbalimbali ndani ya Mkoa wa Rukwa ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi alitembelea miradi ya barabara za lami katika Mji wa Namanyere zilizokamilika na zinazoendelea kujengwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa TARURA alitembelea na kujionea hali ya daraja la Kavunja lililopo Kijiji cha Kirando katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ambapo hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na jinsi ambavyo Ofisi ya Mratibu wa Mkoa wa Rukwa inavyoshughulikia changamoto zilizo jitokeza za menejimenti ya mkataba na usanifu wa daraja hilo. Hivyo, aliahidi kutuma timu ya Wataalam kuja kwenye daraja hilo na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kutatua changamoto hizo.
Akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, kiongozi huyo alitembelea na kujionea hali ya daraja la Kankwale lililopo Kata ya Kankwale ambalo pia limeharibika kutokana na mvua nyingi zilizonyesha na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ambapo aliagiza kuwa ujenzi wa daraja hilo uanze mara moja kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ili kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji zinarejeshwa kwa wananchi.
Naye Kaimu Mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Selemani Mziray amesema kuwa katika Mji wa Namanyere, ujenzi wa barabara za lami zinazotokana na Ahadi za Mhe. Rais, hadi sasa kilomita mbili (2) zimekamilika na kilomita moja (1) ipo katika utekelezaji na itakamilika tarehe 30/08/2020.
‘‘Tunajitahidi ili kuhakikisha miradi hii inayotokana na Ahadi za Mhe. Rais inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili wananchi waweze kunufaika”, alisema Mhandisi Mziray.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake mkoani Rukwa, Mtendaji Mkuu wa TARURA alifanya kikao kazi na Mameneja wote wa TARURA waliopo kwenye Halmashauri zote zilizopo kwenye Mkoa wa Rukwa ili kutoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujadili namna ya kuendelea kurejesha mawasiliano kwa maeneo yaliyoathiriwa sana na mvua.