Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Royal Tour Yaendelea Kupaisha Idadi ya Watalii Tanzania
Mar 10, 2024
Royal Tour Yaendelea Kupaisha Idadi ya Watalii Tanzania
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Mobhare Matinyi akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu baada ya mvua kubwa za El nino katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti leo Machi 10, 2024 katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dodoma.
Na Lilian Lundo (Maelezo)i

Idadi ya watalii imeendelea kuongeza hapa nchini, ikiwa ni matokeo ya filamu ya Royal Tour, ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa mshiriki mkuu.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amesema hayo leo Machi 10, 2023 jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu baada ya mvua za El Nino katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

“Idadi ya watalii wanaokuja nchini imekwenda juu kupita malengo makubwa yaliyowekwa kwa mwaka huu wa fedha. Taarifa ya mafanikio hayo ni kwamba, ingawa makadirio ya idadi ya watalii kwa hifadhi zote za TANAPA kwa mwaka 2023/24 yalikuwa 1,387,987 lakini mpaka kufikia Februari 2024 (miezi nane tu kuanzia Julai 2023), jumla ya watalii 1,451,383 wameshaingia huku Serengeti ikiwa na watalii wengi zaidi,” amesema Bw. Matinyi.

Watalii hao wametoka maeneo mbalimbali ya dunia, ambapo watalii kutoka nje ya nchi za Afrika Mashariki ni 749,365, watalii wageni lakini wakaazi wa nchini Tanzania ni 10,531, watalii wa Afrika Mashariki 230,785 ambapo kati ya hao watalii 127,650 ni Watanzania, pamoja na wafanyakazi wa hoteli, kambi na madereva 460,702.

Kwa upande wa miundombinu amesema kuwa, hifadhi za taifa 21 zilizo chini ya TANAPA zina barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 16,470.6 ambapo Serengeti peke yake ina jumla ya kilomita 3,176, ikiwa  ni hifadhi yenye mtandao mrefu zaidi wa barabara ambazo ni za udongo ama changarawe. 

“Barabara hizi zimegawanyika katika barabara kuu zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) na kundi la pili la barabara ndogondogo zilizo chini ya TANAPA yenyewe. Serengeti pia ina viwanja vidogo vya ndege (airstrips) vipatavyo saba ambavyo ni Serengeti, Kogatende, Lobo, Lamai, Grumeti, Kusini na Fort Ikoma,” amesema Bw. Mobhare.

Aidha, amesema kuwa TANAPA huzitunza barabara hizo na viwanja vya ndege ili kuhakikisha watalii wanaendelea kuingia hifadhini, ambapo hutumia wataalam wake pamoja na vifaa vyake. Kwa mujibu wa sera yake ya uhifadhi, TANAPA hutumia changarawe kutoka ndani ya hifadhi kwa ajili ya matumizi endelevu, kupunguza gharama na kuepuka kuingiza mimea-vamizi ambayo huharibu malisho ya wanyama na pia kuleta magonjwa ya mimea.

“Pale ilipotokea changamoto ya mvua za El Nino kulitokea mafuriko makubwa hifadhini kiasi cha kufunika barabara kuu zinazoleta watalii. Uharibu ulikuwa mkubwa. Hivyo basi, TANAPA ilichukua hatua za haraka za awali za kuzifanyia matengenezo barabara hizo ili kuhakikisha kwamba wageni wanaendelea kutalii na usafirishaji haukwami,” amesema Bw. Matinyi.

Ameendelea kusema kuwa, TANAPA katika hatua za awali imekamilisha matengenezo na sasa barabara hizo zinapitika na watalii wanaendelea kupata huduma zinazostahili. Amesema, “Hakuna changamoto kubwa iliyotokea kwenye upande wa viwanja vidogo vya ndege saba vilivyopo zaidi ya maji kujaa kwenye baadhi ya maeneo ya kuegeshea ndege. Hivyo baada ya maji hayo kukauka, huduma ziliendelea kwa usalama”.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa miaka mitano mfululizo. Serengeti ni maarufu zaidi kwa tukio la uhamaji wa wanyama aina ya nyumbu ambapo kila mwaka nyumbu wapatao milioni 1.5 hutumia miezi kumi wakizunguka ndani ya hifadhi ya Serengeti na kisha kwenda nchi jirani na kurejea. Katika uhamaji huo tukio la kusisimua zaidi ambalo ndilo huvuta watalii wengi ni lile la kuvuka mto Mara pamoja na matawi yake.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi