Bohari ya Dawa (MSD) imejivunia kupanua wigo na ubora wa huduma zake katika kuzalisha dawa, kununua, kutunza na kusambaza kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo ni hospitali, zahanati na vituo vya afya kote nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Mavere Tukai wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya MSD katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mwelekeo wake, leo Machi 19, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
"Kwa mwaka huu 2024/2025 tumefikia kuhudumia hadi vituo vya kutolea huduma za afya 8,466 ikilinganishwa na mwaka 2021/2022 vilikuwa vituo 7,079 katika kipindi kama hicho, ni takribani ongezeko la asilimia 20," amesema Bw. Tukai
Pia ameeleza kuwa, vifo vya mama wanaojifungua vimepungua kutokana na upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba kwenye sehemu zote za kutolea huduma za afya.
"Vifo vya mama wanaojifungua vimepungua kutoka 556 mwaka 2016/2017 hadi vifo 104 mwaka 2021/2022, hii pia inajumuisha upatikanaji wa mashine za kisasa katika matibabu," ameongeza Bw. Tukai
Vile vile, ameeleza kuwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya vimepatiwa vifaa tiba na dawa za kutosha.
"Mwaka 2021 tulisambaza vifaa tiba vya shilingi bil. 18 tu, 2022/2023 vya shilingi bil. 56, 2023/24 vya shilingi bil. 193 na kuanzia Julai, 2024 hadi sasa ndani ya miezi saba tu tumeshasambaza vifaa tiba vya shilingi bil 109, hadi tunamaliza Mwaka wa Fedha 2024/2025 tutakuwa tumefika mbali sana," alisema Tukai
Upatikanaji wa dawa, vifaa tiba vinavyohusisha mashine za kisasa katika matibabu ya magonjwa mbalimbali yanaifanya MSD kujivunia mafanikio hayo ambayo yanafanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.